Trump amshutumu Obama kwa “uhaini” ataka ashtakiwe
29 Julai 2025Rais wa Marekani Donald Trump ameibua tuhuma nzito dhidi ya mtangulizi wake Barack Obama, akisema alihusika katika "njama ya uhaini” kuhusiana na uchunguzi wa kuingilia kwa Urusi kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2016. Kauli ya Trump imekuja baada ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa, Tulsi Gabbard, kuweka hadharani nyaraka alizodai zina ushahidi wa njama hiyo, madai ambayo yamepingwa vikali na chama cha Democratic na wachambuzi wa kisiasa.
Trump adai kesi ya Jeffrey Epstein Ni “Uongo Mpya” wa wapinzani Wake
Trump, ambaye mara kwa mara amekuwa akimshambulia Obama kwa jina, hakuwahi kufikia hatua ya kumshutumu waziwazi kwa madai ya uhalifu tangu alipoingia tena madarakani mwezi Januari.
Safari hii, alikumbatia haraka kauli za Gabbard, aliyedai kuwa maafisa waandamizi wa utawala wa Obama walitengeneza ripoti ya kiintelijensia kwa makusudi ili kupotosha ukweli. "Ukweli uko wazi. Ana hatia. Huu ulikuwa uhaini. Walijaribu kuiba uchaguzi,” alisema Trump bila kutoa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha madai yake.
Kauli za Tulsi Gabbard
Gabbard alifafanua kuwa nyaraka mpya zilizotolewa zinaonyesha namna timu ya Obama ilivyounda tathmini ya ujasusi wakijua kuwa si ya kweli.
"Kuna ushahidi usiopingika unaoonyesha jinsi Rais Obama na timu yake ya usalama walivyoelekeza kutungwa kwa tathmini ya ujasusi ambayo walijua si ya kweli. Walijua itasaidia kusambaza hadithi ya kupangwa kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa 2016 ili kumsaidia Trump kushinda, na wakaipatia umma kana kwamba ni ya kweli,” alisema Gabbard.
Kwa upande wake, msemaji wa Obama, Patrick Rodenbush, alikanusha madai ya Trump, akisema "tuhuma hizi za ajabu ni upuuzi na jaribio dhaifu la kupotosha mjadala.” Chama cha Democratic pia kimepuuzilia mbali madai hayo, kikiyataja kama siasa chafu zisizo na msingi.
Changamoto za kisheria
Wataalamu wa sheria wanasema kuwa hata kama madai hayo yangekuwa na ushahidi, mashtaka dhidi ya rais wa zamani yangekumbwa na vikwazo vingi vya kisheria. Profesa James Sample wa Chuo Kikuu cha Hofstra anasema: "Hakuna jambo la urais zaidi kuliko kuchunguza uingiliaji wa mataifa ya nje katika demokrasia ya Marekani. "
"Kwa hivyo, Trump anataka kufungua mashtaka ambayo yanapingana na kinga ya urais aliyoiweka mwenyewe kupitia Mahakama ya Juu. Iwapo mahakama hiyo itakuwa na msimamo thabiti, italazimika kutamka kuwa Obama ana kinga dhidi ya madai ya Tulsi Gabbard.”
Tuhuma hizi zinakuja licha ya ripoti za awali za idara za intelijensia za Marekani na kamati ya Seneti mwaka 2020, zilizothibitisha kwamba Urusi ilijaribu kuathiri uchaguzi wa 2016 kwa njia ya mitandao ya kijamii na tovuti ya WikiLeaks, lakini haikufanikiwa kubadilisha matokeo ya kura. Hata hivyo, Trump na wafuasi wake wameendelea kupinga hitimisho hilo na kulihusisha na njama za kisiasa dhidi ya urais wake. Mwanasheria Mkuu Pam Bondi amesema kutakuwa na "kikosi kazi maalum” kitakachopitia ripoti ya Gabbard kuhusu Obama.
Hata hivyo, hakutangaza kuanzishwa kwa uchunguzi wa moja kwa moja dhidi ya rais huyo wa zamani, badala yake akibainisha kuwa wanasubiri kuchunguza "hatua zinazowezekana za kisheria zinazofuata.”