Trump amkaripia Netanyahu kwa shambulizi la Qatar
10 Septemba 2025Katika tukio la nadra, Rais wa Marekani Donald Trump amemkaripia waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas nchini Qatar, huku akisisitiza kuwa hakuhusika katika shambulio la mshirika mmoja wa karibu wa Marekani dhidi ya mwenzake.
Trump alisema alijaribu lakini "kwa bahati mbaya, alichelewa" kulizuia shambulizi la Israeli nchini Qatar, wakala muhimu katika mazungumzo kati ya Israeli na Hamas kuvifikisha mwisho vita vya Gaza. "Huu ulikuwa uamuzi uliofanywa na Waziri Mkuu Netanyahu, haukuwa uamuzi nilioufanya," Trump alisema katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.
"Ninaiona Qatar kama mshirika mwenye nguvu na rafiki wa Marekani, na ninajisikia vibaya sana kuhusu eneo la mashambulizi," alisema -- akiongeza kuwa kuwaangamiza Hamas bado ni "lengo linalostahili."
Katika taarifa ambayo kwa kiasi kikubwa ilisisitiza ile iliyotolewa awali na Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt, Trump aliangazia uharibifu unaowezekana kwa juhudi zake za kuvifikisha mwisho vita vya Gaza.
"Kulipua kwa mabomu moja kwa moja ndani ya Qatar, Taifa huru na Mshirika wa karibu wa Marekani, ambayo inafanya kazi kwa bidii na kwa ujasiri kuchukua hatua za hatari na sisi ili kuleta amani, haiendelezi malengo ya Israeli au Amerika," Trump alisema.
Qatar imesema itaendelea na juhudi za upatanishi kutafuta makubaliano ya usitishaji mapigano na kuachiwa huru kwa wafungwa huko Gaza, licha ya shambulizi hilo lililowaua watu sita, akiwemo mtoto wa kiume wa mpatanishi mkuu wa Hamas Khalil al-Hayya na afisa wa usalama wa Qatar.
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema Qatar ina haki ya kujibu shambulizi hilo la wazi, akilieleza kuwa ni wakati muhimu kwa eneo hilo. Ameongeza kusema hakuna kitakachowazuia kuendelea na jukumu hilo la upatanisho kwa masuala mbalimbali yanayoendelea katika eneo lao.
Shambulizi la Israel nchini Qatar halikubaliki
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amelaani vikali shambulizi la Israel dhidi ya Hamas nchini Qatar. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Stefan Kornellius amesema Merz, katika mazungumzo ya simu na emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani, alielezea kuhusu ukiukwaji wa uhuru na mipaka ya Qatar kupitia shambulizi la Israel akisema halikubaliki. Wakati huo huo,
Merz amesifu juhudi za upatanishi za Qatar kutafuta usitiishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuachiwa huru kwa mateka. Merz ametahadharisha kwamba vita vya Gaza havitakiwi viruhisiwe kuenea katika eneo pana la Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Italia imeelezea mshikamano wake na Qatar kufuatia shambulizi la Israel dhidi ya Hamas huko Doha na imetoa wito wa kuepusha machafuko zaidi katika eneo hilo.
Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni ameelezea masikitiko yake kwa emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani na Qatar, akisisitiza msaada wa Italia kwa juhudi za kuvifikisha mwisho vita vya Gaza. Meloni pia amesema Italia inaendelea kupinga aina zote za kuchochea zaidi machafuko yanayoweza kuukoleza mzozo wa Mashariki ya Kati.
Wakati haya yakiarifiwa, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linafanya kikao cha dharura hivi leo kufuatia shambulizi la Israel lililowalenga maafisa wa Hamas nchini Qatar. Duru za kidiplomasia zimesema mkutano huo utafanyaika mida ya saa tisa mchana saa za New York, kufuatia ombi la Algeria na Pakistan, miongoni mwa nchi nyingine.