Trump amkaripia Netanyahu kuhusu mashambulizi ya Qatar
10 Septemba 2025Rais Donald Trump wa Marekani amemkemea waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika hatua ya nadra kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas, huku akisisitiza hakuwa na jukumu lolote katika shambulizi hilo lililofanywa na mmoja wa washirika wake wa karibu dhidi ya mwingine.
Trump amesema alijaribu kulizuia shambulizi hilo lakini alikuwa ameshachelewa, akiongeza kwamba ni uamuzi uliopitishwa na Netanyahu na wala si yeye.
Qatar, mpatanishi muhimu katika mazungumzo biana ya Israel na Hamas katika kutafuta njia ya kuvifikisha mwisho vita vya Gaza, imesema itaendelea na majukumu yake ya upatanishi licha ya shambulizi hilo.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na waziri wake wa mambo ya nje Johann Wadephul wamesema shambulizi la Israel nchini Qatar halikubaliki.
Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni ameelezea masikito yake kwa Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani na Qatar nzima, akisisitiza msaada wa Italia kwa juhudi zote za kuvifikisha mwisho vita vya Gaza.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linafanya kikao cha dharura hivi leo kujadili shambulizi la Israel dhidi ya maafisa wa Hamas nchini Qatar.