Trump amkaribisha Starmer bila ahadi ya usalama kwa Ulaya
28 Februari 2025Waziri mkuu huyo wa Uingereza aliitumia ziara yake hiyo mjini Washington kujaribu kumshawishi mwenyeji wake asiitelekeze Ukraine wakati huu Trump anaposaka suluhisho la haraka la kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka mitatu sasa baada ya Urusi kumvamia jirani yake huyo Februari 2022.
Starmer alimwambia Trump kwamba licha ya umuhimu wa juhudi zake kwa amani ya Ukraine na Ulaya kwa ujumla, lakini lazima zifanyike kwa usahihi ili kutokumzawadia Rais Vladimir Putin wa Urusi badala ya kumuadhibu.
Soma zaidi: Starmer afanya ziara ya kukutana na Trump Washington
"Tumejadiliana mpango wa kufikia amani ambayo ni imara na ya haki, ambao Ukraine itasaidia kuupa sura, ambao umejengeka kwenye kupata nguvu za kumzuwia Putin asirejee kutaka zaidi. Ninashirikiana na viongozi wengine wa Ulaya kwenye hili, na niko wazi kwamba Uingereza iko tayari kutuma wanajeshi ardhini na ndege angani kuunga mkono mpango huu, kwa kushirikiana na washirika wetu, kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha amani inadumu." Alisema Starmer.
Kwa upande wake, Trump alisema kwamba mazungumzo ya kukomesha vita hivyo yanaendelea vyema lakini pia alionya kwamba kuna fursa finyu sana ya kupatikana makubaliano.
"Nadhani tutakuwa na amani iliyofanikiwa sana, na nadhani itakuwa amani ya kudumu. Na nadhani makubaliano yatapatikana haraka sana. Lakini endapo hayakupatikana haraka, basi huenda yasipatikane milele." Alisema Trump.
Kauli za mashaka
Baadhi ya kauli za Trump kwenye ziara hiyo ya Starmer zilionekana kuzidi kuongeza wasiwasi wa Ulaya, kama pale alipoelezea imani yake kwamba Rais Putin hatotaka kuanzisha upya vita endapo makubaliano yakifikiwa sasa.
"Nadhani ataheshimu kauli yake. Nimezungumza naye, nimejuwana naye kwa muda mrefu sasa, tulilazimika kulishughulikia suala la udukuzi wa Kirusi pamoja." Alisema Trump.
Soma zaidi: Kansela Scholz akutana na Starmer huko Uingereza
Kwa kutumia kwake neno la "udukuzi wa Kirusi", Trump alikuwa akimaanisha uchunguzi maalum wa Shirika la Ujasusi la Marekani, FBI, na Wizara ya Sheria ya nchi hiyo kuamua endapo kampeni ya urais ya Trump ya mwaka 2016 ilisaidiwa na udukuzi wa barua-pepe za Democrat, lakini wakadunguwa kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha ushirikiano wa Trump na Moscow.
Alipoulizwa Starmer juu ya mtazamo wake kwa uaminifu wa Putin endapo patafikiwa makubaliano ya kusitisha vita na Ukraine, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadhani ikiwa rais huyo wa Urusi atakuwa mkweli.
Ulaya haina uhakika na Trump
Ziara ya Starmer inafuatia ile ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye alikuwapo mjini Washington mapema wiki hii kwa lengo hilo hilo la kumshawishi Trump asiitelekeze Ukraine inayokabiliana na uvamizi wa Urusi.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alitazamiwa naye kukutana na Rais Trump siku ya Ijumaa (Februari 28) katika Ikulu ya White House. hapana shaka naye akipigania msaada wa Marekani kwenye vita vyake dhidi ya Urusi.
Soma zaidi: Uingereza yaahidi kuihakikishia Ukraine usalama
Shinikizo la Starmer na Macron ni muakisiko wa wasiwasi unaozidi kukuwa kote barani Ulaya kwamba shinikizo la Trump la kukomesha vita hivyo linaashiria utayari wake wa kumkubalia mambo mengi Rais Putin, hata kwa gharama ya maslahi na usalama wa Ukraine na Ulaya nzima.