Trump amkaribisha Netanyahu Ikulu ya White House
8 Julai 2025Rais wa Marekani Donald Trump amekutana na mgeni wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington huku ajenda kuu ya mazungumzo yao ikiwa ni vita vilivyodumu kwa miezi 21 kwenye Ukanda wa Gaza.
Mkutano huo ambao ni wa tatu kati ya viongozi hao wawili katika mwaka huu, umefanyika wakati juhudi zinaendelea kujaribu kuvifikisha mwisho vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Usiku wa kuamkia Jumanne Rais Donald Trump alimkaribisha mgeni wake huyo kwanza kwa chakula cha pamoja na baadaye mazungumzo ambayo rais huyo alimshinikiza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuvimaliza vita huko Gaza.
Nikinukuu maneno yake, Trump amesema "Hamas wanataka kukutana na wanataka kuwepo kwa usitishaji wa mapigano," mwisho wa kumnukuu.
Alipoulizwa na waandishi wa habari ikiwa kama kuna uwezekano suluhisho la kuwepo kwa mataifa mawili, Rais Trump alijibu kwamba hajui na kwamba swali hilo aulizwe Netanyahu.
Netanyahu alijibu kwamba Israel itakuwa na amani na majirani zetu wa Palestina lakini wale ambao hawataki kuiangamiza nchi yake lakini suala la kuleta amani , usalama, nguvu kuu ya usalama, daima inabaki mikononi mwetu, lakini akaongeza kwamba Israel inafanya kazi kwa karibu na Marekani katika kuwatafutia makazi wapalestina wasio na makazi katika nchi nyingine.
Benjamin Netanyahu pia amemkabidhi barua Rais Trump ambayo amesema amewatumia kamati ya tuzo ya Nobel ya kumpendekeza rais Trump kupewa tuzo hiyo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kuleta amani.
Marekani imekuwa mshirika wa kuaminika kwa Israel katika vita vyake huko mashariki ya kati, hivi karibuni waliisaidia Israel kwa kulipua vituo muhimu vya nyuklia vya Iran.
Trump: Nina imani vita vya Israel na Iran vimemalizika
Rais Trump pia amesema ana matumaini kwamba vita kati ya Israel na Iran vimefikia tamati na kwamba muda ukifika ataiondolea vikwazo Iran. Alipozungumzia kuhusu kubadilisha utawala wa Iran, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hilo suala liko juu ya wairan wenyewe kuamua hatma ya nchi yao.
Katika upande mwingine, mazungumzo kati ya wajumbe wa Israel na Hamas yamekamilika mjini Doha bila "mafanikio," afisa wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wajumbe hao bado wataendelea kwa mazungumzo mengine.
Mjumbe maalum wa Trump Steve Witkoff anatarajiwa kufika mjini Doha kujiunga kwa mazungumzo hayo baadaye wiki hii katika juhudi za usitishaji mapigano.
Siku ya Jumapili Rais Trump alisema kwamba upo uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka na kupatikana kwa suluhisho la usitishaji wa vita kati yao na Hamas mwishoni mwa wiki hii.
Kati ya mateka 251 waliochukuliwa na wanamgambo wa Kipalestina wakati wa shambulio la Hamas la Oktoba 2023 ambalo lilianzisha vita, 49 bado wanashikiliwa Gaza, wakiwemo 27 jeshi la Israel linasema wamekufa.