Trump asema 'ndoto ya Marekani haizuiliki'
5 Machi 2025Kwenye hotuba yake kwa kikao cha Pamoja cha mabaraza yote mawili ya bunge – Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti, Trump amejivunia siku zake 44 za kwanza madarakani, akisema ni "mwezi wa kwanza wenye mafanikio zaidi" ya muhula wowote wa urais wa Marekani katika historia.
Mada ya Trump ilikuwa ni "kuianzisha upya ndoto ya Marekani." Rais amesema kuwa ndoto ya Marekani "haizuiliki" na kwamba nchi hiyo inarejesha imani yake anapoanza wake wa muhula wa pili.
Kuhusu biashara, ameitetea kampeni yake ya kuziwekea ushuru bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka kwa washirika wakuu wa Marekani.
Hayo ni licha ya wasiwasi kuwa huenda hatua hiyo ikaongeza bei za bidhaa na huduma na kuathiri ukuaji uchumi. Rais amesema washirika wake wakiamua kuweka ushuru kwenye bidhaa za Marekani, nayo Marekani itajibu kwa kuweka ushuru. Kama wataikata kodi Marekani, nayo Marekani itawakata kodi.
Wakati akianza hotuba yake, Trump alikabiliwa na wakati mgumu kutoka kwa Wademocrat waliokuwa wakimzomea. Warepublican walionekana kushangilia kila wakati kwa kuinuka vitini na kupiga makofi.
Ameliambia Bunge kuwa anafanya juhudi za kumaliza vita vya Urusi na Ukraine. Baada ya msuguano wa hadharani na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Trump alisitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Aidha amesema baadae wiki hii, atatangaza upanuzi wa uzalishaji wa madini muhimu nchini Marekani. Trump ametangaza mipango yake ya kushinikiza kuwachiwa mateka waliochukuliwa na Hamas kutoka Israel na kushikiliwa katika Ukanda wa Gaza.
Kuhusu masuala ya ndani, Hatimaye ameliomba Bunge fedha za kuufanikisha mpango wake wa kuwafukuza nchini wahamiaji wengi wasio na vibali, ambao baadhi yao tayari serikali yake imewahamishia Guantanamo Bay.
Kabla ya hotuba hiyo, Trump na mke wake Melania Trump, pamoja na mshauri wa rais bilionea Elon Musk, waliondoka Ikulu ya White House kwa safari fupi ya kuelekea jengo la Capitol. Makamu wa Rais JD Vance na mawaziri wa Trump pia walihudhuria.
Akisaidiwa na Musk, Trump ameshughulikia kwa haraka mageuzi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kuhusu urasimu wa serikali kuu ambayo yamesababisha kufutwa kwa maelfu ya kazi, kufungwa kwa mashirika yote na kukatwa kwa misaada ya kigeni.
Amerejea bungeni, miaka minne tu baada ya kuondoka madarakani kwa aibu baada ya wafuasi wake kuvamia jengo hilo la Capitol wakipinga kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2020.
Trump mwenye umri wa miaka 78, anarejea kama rais mwenye nguvu zaidi wa chama cha Republican katika miongo kadhaa, akiwa na kura nyingi za umaarufu huku Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti yote yakidhibitiwa na chama cha Republican.
Waandamanaji walijitokeza viwanjani, nje ya mabunge ya majimbo na maeneo mengine ya umma wakati Trump akijiandaa kwa hotuba yake. Maandamano hayo yalipangwa na vuguvugu la 50501. Waandamanaji wanapinga hatua mbalimbali zenye utata za Trump, kuanzia ushuru, hadi msimamo wake kuhusu vita vya Ukraine, na hatua za Idara ya Ufanisi wa Serikali inayoongozwa na Elon Musk (DOGE). Matukio yalipangwa kufanyika siku nzima katika majimbo yote 50.
afp, dpa, reuters, ap