Trump akutana na kiongozi wa Syria mjini Riyadh hii leo
14 Mei 2025Rais wa Marekani Donald Trump aliyeko ziarani huko Mashariki ya Kati amekutana leo na kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa katika siku yake ya mwisho mjini Riyadh, Saudia arabia baada ya hapo jana kuapa kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Akizungumza mjini Riyadh, Trump amemtaka Sharaa kurekebisha uhusiano kati yaSyria na Israel ambayo imekuwa na wasiwasi na kiongozi huyo kwa sababu za uhusiano wake wa zamani na kundi la kigaidi la Al Qaeda.
Soma zaidi: Marekani na Saudi Arabia zatia saini makubaliano ya uchumi, ulinzi
Jana Jumanne, Kiongozi huyo wa Marekani alisema utawala wake wake umedhamiria kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Trump "Syria imeshuhudia masaibu na vifo vingi, kuna serikali mpya ambayo nina matumaini itafanikiwa kuleta utulivu wa nchi na kudumisha amani. Hilo ndilo tunalotaka kuona huko Syria. Wamekuwa sehemu yao ya uharibifu, vita na mauaji kwa miaka mingi. Ndiyo maana utawala wangu tayari umechukua hatua za kwanza za kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Marekani na Syria, kwa mara ya kwanza kwa zaidi muongo mmoja uliopita''.
Rais Trump pia amekutana na viongozi wengine wa mataifa ya Ghuba mjini Riyadh, kabla ya kusafiri kuelekea Qatar baadaye hii leo.