Rais Trump akatisha ghafla mkutano wa kilele wa G7
17 Juni 2025Rais Donald Trump wa Marekani amelazimika kukatisha mkutano wa kilele wa kundi la nchi saba tajiri kiviwanda G7 unaofanyika nchini Canada,akisema kuwa ataondoka mapema na kurejea Washington, kutokana na hali inayoendelea Mashariki ya Kati.
Katika mkutano huo, Trump alionya vikali kwamba Iran inahitaji kuzuia mpango wake wa nyuklia kabla haijachelewa, huku akitoa tahadhari watu kuondoka mara moja kutoka mji mkuu wa Tehran.
Wakati wa picha ya pamoja jana jioni na viongozi wengine wa G7, Trump alinukuliwa akisema ni muhimu kwake kurejea haraka jijini Washington. Hiyo inamaanisha kuwa Trump hatoshiriki mikutano ya leo Jumanne ambayo itajadili vita vinavyoendelea nchini Ukraine na masuala ya biashara ya kimataifa.
Viongozi wa G7 wamekusanyika nchini Canada kwa lengo la kutafuta suluhu ya mizozo ya kimataifa, lakini wamejikuta wakitatizwa na mzozo mpya uliozuka wa mapigano kati ya Israel na Iran huku wasiwasi ukitanda juu ya kupanuka kwa mgogoro huo.