Trump akana tena barua ya Epstein: "Siyo sahihi yangu"
10 Septemba 2025Rais wa Marekani, Donald Trump, amekanusha kwa mara nyingine madai kwamba aliandika barua ya utata iliyoibuliwa kutoka mali ya aliyekuwa mfanyabiashara Jeffrey Epstein, akisisitiza kuwa sahihi iliyomo si yake.
Barua hiyo, ambayo iliwekwa katika kitabu cha kumbukumbu cha sherehe ya kuzaliwa ya Epstein mwaka 2003, ilijumuisha mchoro wa mwanamke alie uchi ambapo sehemu ya nyeti ilibandikwa sahihi inayodaiwa kuwa ya Trump.
Taarifa za kwanza kuhusu kuwepo kwa barua hiyo ziliripotiwa na Wall Street Journal mwezi Julai, jambo lililomfanya Trump kufungua kesi ya madai ya mabilioni ya dola dhidi ya gazeti hilo na wamiliki wake kwa madai ya kashfa.
Jumatatu wiki hii, Kamati ya Usimamizi ya Bunge la Marekani (House Oversight Committee) ilichapisha nakala ya kitabu hicho pamoja na nyaraka zingine zilizokusanywa kutoka mali ya Epstein.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, Trump alisema: "Siyo sahihi yangu na wala siyo mtindo wangu wa kuandika. Wale wanaonifuatilia kwa muda mrefu wanajua siyo lugha yangu. Ni upuuzi mtupu.”
Ikulu ya White House yajibu
Barua hiyo ina mazungumzo mafupi kati ya "Donald” na "Jeffrey,” ambapo Trump anadaiwa kuandika sentensi tata kwamba "enigmas never age”. Barua ilimalizika kwa salamu za heri ya kuzaliwa.
Kwa upande wake, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, alisisitiza kwamba Rais hakusaini wala kuandika barua hiyo na akasema White House iko tayari kwa uchunguzi wa kitaalamu wa sahihi hiyo.
Leavitt alisema: "Sahihi ya rais ni moja ya maarufu zaidi duniani kwa miaka mingi. Ni wazi kabisa kwamba hii siyo kazi yake.”
Gazeti la New York Times hata hivyo liliibua mashaka baada ya kuchapisha barua nyingine zilizotiwa saini na Trump mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000, ambazo zinafanana sana na sahihi iliyoko kwenye barua ya Epstein.
Mashaka kuhusu kifo cha Epstein
Epstein, aliyekuwa mfanyabiashara mwenye mtandao mkubwa wa marafiki mashuhuri duniani, alihukumiwa kwa makosa ya kingono na alikutikana amefariki gerezani New York mwaka 2019 akiwa anasubiri kesi ya ulanguzi wa wasichana wadogo.
Kifo chake kilitangazwa kuwa ni kujiua, lakini mashaka na nadharia za njama zimeendelea kuzunguka tukio hilo, hali iliyosababisha Wamarekani wengi kuamini serikali inaficha ukweli.
Utafiti mpya wa Reuters/Ipsos unaonyesha kuwa asilimia 65 ya Wamarekani wanaamini serikali inaficha taarifa muhimu kuhusu kifo cha Epstein, huku asilimia 72 wakisema kuna uficho kuhusu wateja wake waliotajwa katika kesi za ulanguzi wa kingono.
Hata hivyo, kura hiyo pia ilileta faraja ndogo kwa Trump, kwani idadi ya Warepublican wanaounga mkono jinsi anavyoshughulikia suala la Epstein imeongezeka kutoka asilimia 35 mwezi Julai hadi asilimia 44 sasa.
Athari za kisiasa
Kwa upande wa kisiasa, wapinzani wa Trump wamekuwa wakitumia uhusiano wake wa zamani na Epstein kama silaha dhidi yake, wakati yeye na wafuasi wake wakijaribu kulipuuza sakata hilo kama njama za kidemokrasia.
Wachambuzi wanasema mjadala huu unaweza kuendelea kuwa kikwazo kwa kampeni za Trump, hasa iwapo uchunguzi wa maandishi utabaini sahihi hiyo ni halisi.