Trump akabiliwa na shinikizo, sakata la Epstein
24 Julai 2025Hayo ni baada ya wizara ya sheria kutangaza wiki mbili zilizopita kuwa kesi hiyo imemalizika na kwamba hakuna taarifa zaidi zinazopaswa kuwekwa bayana. Hata hivyo baadhi ya wabunge wanataka ukweli uwekwe hadharani kuhusu kesi hiyo.
Sakata hilo la Epstein limesababisha hali ya vuta nikuvute katika Baraza la Wawakilishi la Marekani ambapo spika wa Bunge kutoka chama cha Republican Mike Johnson anajaribu kuzuia kura inayohofiwa mno na utawala wa Donald Trump kwa kutaka kuwapeleka wabunge kwenye mapumziko ya mapema.
Mbunge wa chama cha Republican Thomas Massie akishirikiana na wabunge wengine wa Democrats wanalenga kuwasilisha muswada wa kulipigia kura azimio ambalo litaruhusu kuchapishwa kwa hati za mahakama juu ya kesi ya Jeffrey Epstein.
Wizara ya sheria ya Marekani ilikosolewa vikali kwa kushindwa wiki iliyopita kutoa nyaraka zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu kuhusu kesi ya usafirishaji wa kingono ya Jeffrey Epstein. Trump alijibu ukosoaji huo huku akiwatuhumu marais wa zamani Barack Obama na Joe Biden, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI James Comey kwa kughusi nyaraka hizo huku akiwalaumu wa Demokrati kwa kuanzisha kile alichokiita "uongo mpya".
Baada ya Trump kuingia madarakani kwa muhula wa pili, utawala wake uliahidi kukuchapisha waziwazi nyaraka zote kuhusu kesi ya Epstein. Lakini Mwanasheria Mkuu wa Marekani Pam Bondi alitangaza mnamo Julai 7 kwamba hakuwa na chochote cha kuchapisha, hatua iliyoukasirisha umma wa Marekani na tangu wakati huo, Trump amekuwa akijaribu kudhibiti kashfa hiyo.
Trump akosolewa hadi na wafuasi wake
Trump amekuwa akikosolewa hadi na wafuasi wa kampeni yake inayofahamika zaidi kama "MAGA" (Make America Great Againt) wakisema shutuma hizo kwa watangulizi wake ni hatua ya kujaribu kuuficha ukweli kuhusu sakata hilo. Trump aliwashambulia wafuasi wake na kusema wameamini "uongo huo” na kwamba hataki tena uungwaji mkono kutoka kwa wale aliyowaita "watu dhaifu.”
Hata hivyo licha ya majaribio ya kutaka kusawazisha kesi hii, Spika wa Bunge la Marekani Mike Johnson amesema kesi ya Epstein si uongo na anataka sheria ifuate mkondo wake.
"Tunataka uwazi kamili. Tunataka kila mtu aliyehusika kwa njia yoyote na uovu huu wa Epstein awajibishwe haraka iwezekanavyo mbele ya mahakama. Tunataka sheria iwakabili "
Je, unamfahamu Jeffrey Epstein?
Kwa miaka mingi, Jeffrey Epstein alikuwa mfanyabiashara tajiri wa Marekani na msimamizi wa mali za mabilionea wengi lakini pia rafiki wa watu wengi mashuhuri akiwemo Trump . Alipatikana na hatia ya uhalifu wa kingono na kisha kufungwa jela akisubiri kusikilizwa kwa kesi iliyomkabili ya kusafirisha wasichana wadogo.
Epstein alifariki mwaka 2019 akiwa jela katika kile kilichotajwa kuwa alijiua, kitendo kilichozidisha nadharia ya njama dhidi yake na iliyoendelezwa kwa muda mrefu kwamba alikuwa akiongoza mtandao wa kimataifa wa usafirishaji wa watoto kwa ajili ya vitendo vya unyanyasaji wa kingono na kwamba watu wengi mashuhuri walifanya kila waliwezalo ili kuhakikisha hafichui siri zao.
(Vyanzo: AP, AFP, Reuters)