Trump aionya Hamas kuwaachia mateka waliosalia
6 Machi 2025Katika ujumbe kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth, Trump ameitaka Hamas kuwaachia haraka iwezekanavyo mateka wote waliosalia pamoja na kukabidhi miili ya wale waliokufa, akionya kwamba iwapo hilo halitofanyika kundi hilo litasambaratishwa.
Trump amesisitiza kuwa hilo ni onyo la mwisho kwa kundi la Hamas akiapa kwamba ataipatia Israel kila inachohitaji ili "kumaliza kazi" kwenye Ukanda wa Gaza, akiusihi uongozi wa Hamas kuondoka Gaza ikiwa bado wanayo nafasi. Tamko la Trump linafuatia onyo jingine la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliyelitaka kundi hilo kuwakabidhi mateka wote wa Israel au likabiliwe na kile alichokiita "madhara yasiyoweza kufikirika".
Hamas imekosoa kauli ya Trump leo Alhamisi na kusema kuwa vitisho vyake vya mara kwa mara kwa Wapalestina, vinamuunga mkono Netanyahu ili aweze kujiondoa kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuzidisha mzingiro na madhila kwa watu wa Gaza.
Hata hivyo, serikali ya Marekani kupitia msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt imethibitisha bila kutoa maelezo zaidi kwamba Marekani ipo kwenye mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu suala la kuachiliwa kwa mateka.
Soma pia: Viongozi wa Kiarabu waidhinisha mpango kuhusu Ukanda wa Gaza
Kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza limekataa kurefusha awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza ambayo yalimalizika Jumamosi iliyopita na limeitaka Israel kurejea mezani kwa majadiliano ya kina ili kuanzishwa awamu ya pili ya makubaliano hayo ambayo itailazimu Hamas kuwaachia mateka wote waliosalia huku Israel ikitakiwa pia kuondoa kabisa wanajeshi wake huko Gaza.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa amani kwa pande zote
Wanachama watano wa Baraza la Usalama la Umoja Mataifa walitoa wito kwa Israel kuruhusu usambazaji wa msaada ya kibinadamu huko Gaza na kutoa wito kwa pande zote kutafuta njia za kuumaliza mzozo huo. Akisoma taarifa hiyo ya pamoja, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Jay Dharmadhikari alizungumza pia kwa niaba ya mataifa ya Uingereza, Denmark, Ugiriki na Slovenia.
"Waisraeli na Wapalestina wanastahili kuishi bega kwa bega kwa amani na usalama. Tunasisitiza dhamira yetu isiyoyumba kuhusu maono ya suluhisho la mataifa mawili ya kidemokrasia, ambapo Israel na Palestina zitaishi kwa amani ndani ya mipaka iliyo salama na inayotambulika, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa."
Israel imekuwa ikipuuza miito kama hiyo na badala yake imeongeza mbinyo kwa kundi hilo ikiwa ni pamoja na kuzuia uingizwaji wa chakula na mahitaji mengine muhimu huko Gaza, hatua ambayo imekosolewa na mashirika ya kimataifa yakisema kwamba Israel inatumia njaa kama silaha ya kivita.
(Vyanzo: DPA, AP, Reuters, AFP)