Trump ahutubia Kongamano la Uchumi la Dunia mjini Davos
24 Januari 2025Akizungumza kwa njia ya video kutoka Ikulu ya Marekani ya White House katika siku yake ya tatu ofisini, Trump alielezea kuhusu hatua alizochukuwa tangu kuapishwa kwake na kudai kuwa ana jukumu kubwa kwa raia wa Marekani kuleta mabadiliko.
Trump aahidi kodi ya chini kwa uwekezaji nchini Marekani
Rais huyo alitumia mbinu ya kuzawadia na kuadhibu kwa uwekezaji wa kibinafsi nchini Marekani na kusema ikiwa wawekezaji watatengeneza bidhaa zao nchini humo watalipa kodi ya chini lakini kinyume cha hayo, itawabidi kulipa ushuru mkubwa ambao utaelekeza mamia ya mabilioni na hata trilioni za dola kwenye hazina ya nchi hiyo ili kuimarisha uchumi wake na kulipa deni chini ya utawala wake.
Saudi Arabia kuwekeza bilioni 600 nchini Marekani
Trump, ambaye alizungumza Jumatano na mwana mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, pia amesema jana kwamba nchi hiyo inataka kuwekeza dola bilioni 600 nchini Marekani, lakini akaongeza kwamba, atamwomba kiongozi huyo wa Saudi Arabia aongezee pesa hizo hadi trilioni 1, kauli iliyoibua vicheko kutoka kwa washiriki wa mkutano huo wa Davos.
Vita vya Urusi na Ukraine bado ni suala la kipaombele kwa Marekani
Trump, ambaye aliahidi kumaliza vita vya Urusi na Ukraine kabla ya kuingia madarakani, amesema suala hilo bado ni la kipaombele, lakini hakutoa maelezo ya kina ya jinsi atakavyolitekeleza.
Rais huyo wa Marekani, ameuambia umati huo wa Davos kwamba jambo moja muhimu sana ni kwamba angependa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin hivi karibuni na kumaliza vita hivyo.
Mapema katika hotuba yake kwa kongamano hilo, Trump alililaumu kundi la mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC+ kwa kuweka juu bei ya mafuta kwa karibu miaka mitatu ya vita. Uuzaji wa mafuta ndio injini ya kiuchumi inayoendesha uchumi wa Urusi.
Hatua za Trump zaendelea kuibua hisia mseto, Davos
Trump aliongeza kuwa ikiwa bei itashuka, vita vya Urusi na Ukraine vitaisha mara moja, na kusema kwamba OPEC+ inahusika kwa kiasi katika kile kinachoendelea.
Trump aushtumu Umoja wa Ulaya
Trump ameushtumu Umoja wa Ulaya na kusema hauutendei haki Marekani kutokana na sheria zake za kibiashara.
Trump alisema hatavumilia nakisi ya biashara ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Pia aliushtumu Umoja huo wa Ulaya kwa kukataa kununua bidhaa za kilimo na magari kutoka Marekani.
Gumzo la ushirikiano na Trump latawala Jukwaa la Uchumi Duniani
Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Trump alitaja mipango ya kuanzisha ushuru mpya wa 10% hadi 20% kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya na kusema utasaidia kuimarisha viwanda vya ndani na kushughulikia nakisi ya biashara.