Trump: Nyaraka za kesi ya Epstein ni uongo wa wapinzani
17 Julai 2025Rais Donald Trump amejibu ukosoaji kuhusu kushindwa kwa wizara ya sheria ya Marekani kutoa nyaraka zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu kuhusu kesi ya usafirishaji wa kingono ya Jeffrey Epstein.
Siku ya Jumanne, Trump aliwatuhumu Marais wa zamani Barack Obama na Joe Biden, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI James Comey, kwa kughusi nyaraka hizo. Siku iliyofuata, aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social akisema kuwa Democratcs wameanzisha uongo mpya.
Trump aliendelea kusema kuwa baadhi ya wafuasi wake wa zamani wameamini "uongo huo” na kwamba hataki tena uungwaji mkono kutoka kwa "watu dhaifu.”
Duru zinasema wizara ya sheria nchini humo imemfuta kazi Maurene Comey, binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la FBI James Comey, ambaye pia ni mwendesha mashtaka mkongwe aliyeshughulikia kesi ya P "Diddy" na Jeffrey Epstein.