Trump yupo tayari kwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi
7 Septemba 2025Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kuanzisha awamu ya pili ya vikwazo dhidi ya Urusi, hatua inayoweza kulenga mauzo ya nishati ya Moscow na washirika wake.
Hii ni mara ya kwanza Trump kuashiria wazi kwamba yuko karibu kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Urusi au wanunuzi wa mafuta yake kutokana na vita vya Ukraine.
Trump amekuwa akitishia mara kadhaa kuongeza vikwazo lakini amevihold wakati akijaribu kusukuma mazungumzo ya amani. Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ikulu ya White House Jumapili, aliulizwa iwapo yuko tayari kwa "awamu ya pili” ya vikwazo, naye akajibu: "Ndiyo, niko tayari” bila kutoa maelezo zaidi.
Kauli hiyo imekuja wakati Urusi ikizidisha mashambulizi yake makubwa zaidi tangu kuanza kwa vita, ambapo makombora na droni vilishambulia Kyiv na kuua watu wasiopungua wanne. Moto mkubwa ulizuka katika jengo la serikali kuu linalohifadhi baraza la mawaziri katikati ya mji, ikiwa mara ya kwanza linalengwa moja kwa moja.
Trump ameonyesha kukasirishwa na kushindwa kwake kufanikisha kusitisha mapigano, baada ya kuahidi mara nyingi kwamba angehitimisha vita kwa haraka alipoingia madarakani Januari. Wasaidizi wake wanasema awamu mpya ya vikwazo inaweza kulenga wanunuzi wakuu wa mafuta ya Urusi, hususan China na India.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema Jumapili kwamba Washington na Umoja wa Ulaya wanaweza kuweka ushuru wa ziada kwa mataifa yanayonunua mafuta ya Urusi, hatua anayoamini ingeisukuma Moscow "ukingoni mwa kuporomoka” na kumlazimisha Rais Vladimir Putin kukaa meza ya mazungumzo.
Shambulio kubwa Kyiv tangu kuanza kwa vita
Kwa mujibu wa jeshi la anga la Ukraine, Urusi ilirusha zaidi ya droni 810 na makombora 13 kati ya Jumamosi usiku na Jumapili alfajiri, shambulio kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika vita vya miaka mitatu na nusu.
Moto ulionekana ukipanda juu ya paa la jengo la baraza la mawaziri mjini Kyiv, huku huduma za dharura zikihangaika kuzima moto. Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko alisema: "Tutajenga upya majengo, lakini maisha yaliyopotea hatuwezi kuyarejesha. Adui anaterrorize watu wetu kila siku.”
Rais Volodymyr Zelensky aliliita shambulio hilo "uhalifu wa makusudi na njia ya kurefusha vita,” akisema sasa ni wakati wa diplomasia ya kweli. Alizungumza na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye aliahidi kusaidia Ukraine kuimarisha ulinzi wake.
Macron alisema kupitia mtandao wa X kwamba Urusi "inazidi kujifungia kwenye mantiki ya vita na ugaidi.” Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliyaita mashambulizi hayo kuwa "ya uoga,” huku Ursula von der Leyen, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, akimshtumu Putin kwa "kuidhihaki diplomasia.”
Urusi ilikanusha kulenga raia, ikidai ilishambulia kiwanda na ghala la vifaa mjini Kyiv. Lakini mashuhuda na madaktari walisema makumi ya raia walijeruhiwa, akiwemo mama mjamzito wa miaka 24 aliyejifungua mtoto njiti muda mfupi baada ya mashambulizi.
Hasara kubwa na hofu
Mashambulizi ya usiku yaligharimu maisha ya watu zaidi mashariki na kusini mwa Ukraine, ambapo makumi walijeruhiwa. Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ilisema hata wanyama hawakuokoka, ikiripoti kwamba farasi saba waliuawa katika klabu ya michezo ya farasi.
"Dunia haiwezi kusimama kando wakati taifa la kigaidi linaua kila siku—watu na hata wanyama,” wizara hiyo ilisema kwenye mtandao wa X.
Trump, ambaye alikutana na Putin mwezi uliopita huko Alaska katika mkutano ulioshindwa kuleta mafanikio ya kusitisha mapigano, amesema anaendelea kusaka njia ya kuhitimisha vita. Lakini kwa sasa, Urusi bado inadhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine, huku mapambano ya gharama kubwa yakiendelea.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni wamelazimika kuyakimbia makazi yao, likiwa ni vita vya damu zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Wakati huo huo, wawakilishi zaidi ya mataifa 20 ya Ulaya wamethibitisha kuwa wako tayari kusimamia makubaliano yoyote ya amani, wakiwemo waliodokeza uwezekano wa kupeleka wanajeshi ardhini Ukraine.
Majibu ya Marekani na washirika
Mjumbe wa Marekani nchini Ukraine, Keith Kellogg, alisema Jumapili kwamba shambulio la Urusi si ishara ya kutaka kumaliza vita kwa diplomasia. "Urusi inaonekana kuongeza kiwango kwa shambulio kubwa zaidi tangu vita kuanza,” Kellogg aliandika kwenye X.
Kwa upande wa ndani ya Marekani, mjadala unaendelea kuhusu iwapo awamu mpya ya vikwazo vya Trump itasaidia kumlazimisha Putin au itazidisha migawanyiko kati ya Washington na washirika wake wa biashara kama India.
Trump mwenyewe alisema hatua zake za awali, kama vile ushuru wa adhabu kwa bidhaa za India mwezi uliopita, ziligharimu Urusi mamia ya mabilioni ya dola kwa sababu India ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Moscow. "Na bado sijaanza awamu ya pili au ya tatu,” alisema.
Lakini kwa sasa, Ikulu ya White House haijatoa maelezo zaidi juu ya ni hatua gani zinazotazamwa, na iwapo vikwazo hivyo vipya vitaungwa mkono na washirika wote wa Ulaya.
Kwa wengi, hatua ya Trump imeashiria mwelekeo mkali zaidi dhidi ya Moscow, ikibaki kusubiriwa iwapo ataitekeleza au itabaki tishio la kisiasa.
Chanzo: AFPE, RTRE, APE