Polisi wa Kenya waongoza kwa kula rushwa
18 Julai 2025Ripoti hiyo inayochora taswira ya kusikitisha kwa huduma ya utumishi kwa umma, inajiri huku idara hiyo hiyo ikinyooshewa kidole kwa kuhusika na mauaji ya kiholela, utekaji na kutoweka kwa watu na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Polisi waliongoza katika vipengele vya uwezekano wa kukutana na ombi la hongo, kutokea kwa ulipaji hongo halisi na asilimia ya jumla ya hongo zote zilizoripotiwa nchini ikiwa ni asilimia 39. Takwimu hizo zinaamanisha kwamba, kati ya Wakenya 10 waliowasiliana na polisi, zaidi ya saba walikutana na ombi la hongo na angalau watano waliilipa.
Stella Masinde, Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International nchini Kenya anafafanua "Kwanini kama afisa wa polisi nisichukuwe hongo iwapo, sijawajibishwa kwa makosa mazito kama vile mauaji na hata kusababisha ghasia na majeruhi."
Sekta zilizofuata kwa viwango vya juu vya ufisadi ni huduma za ardhi ikiwa na asilimia 45, leseni za magari asilimia 43, mahakama asilimia 40 na usajili wa kiraia asilimia 34.
Ingawa maafisa wa polisi walidai kiasi kidogo cha hongo kwa wastani wa shilingi 6,862 kwa kila tukio, idadi kubwa ya mwingiliano wao na wananchi iliwafanya wabebe karibu asilimia 40 ya hongo zote zilizoripotiwa nchini.
Huduma ya Ardhi na Leseni za magari pia wamo
Kwa upande mwingine, idara ya mahakama ilirekodi kiasi cha juu zaidi cha hongo kwa wastani wa shilingi 18,000, ikifuatiwa na huduma za ardhi shilingi 12,000 na leseni za magari shilingi 10,466. Leseni za biashara ndizo zilizoonyesha ongezeko kubwa zaidi la kiasi cha hongo kutoka shilingi 3,136 mwaka 2017 hadi shilingi 7,563 mwaka 2025. Dkt Bernard Mogesa ni Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Kutetea Haki za Raia nchini Kenya-KNHCR:
Alisema "Tutaendelea vipi kuwekeza katika kutoa huduma za umma kwa njia ya dijitali, kwa serikali kama njia moja ya kupunguza hongo ili kupata huduma!"
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa athari za hongo zilionekana zaidi katika mwingiliano kati ya wananchi na polisi, ambapo zaidi ya nusu ya waliolipa hongo walihisi kwamba wasingepata huduma yoyote kama hawangalipa. Ili kukabiliana na janga hili la hongo, ripoti ilihimiza Huduma ya Polisi Nchini kutekeleza kwa dharura mapendekezo ya Ripoti za Mageuzi ya Polisi za mwaka 2009 na 2022.
Aidha, ilizitaka mahakama kuweka mifumo madhubuti ya wafichuzi wa taarifa na kushughulikia kesi za ufisadi kwa uharaka na haki. Mwaka 2019, Idara ya Mahakama iliongoza kwa ufisadi nchini Kenya.