"Tishio la Iran halina msingi"
6 Juni 2006Mwakilishi wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, anaitembelea Iran kuipelekea pendekezo la Umoja huu linalolenga kumaliza mzozo juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran. Gazeti la “Leipziger Volkszeitung” linaona hii ni mtihani wa mwisho. Limeandika:
“Ikiwa rais wa Iran, Mahmud Ahmadinedjad anakataa pendekezo hili, anaonyesha kwamba kwa kweli hajali mzozo utatuliwe. Hivyo ni wazi kwamba mzozo huu hauhusishi matumizi ya nishati ya kinyuklia kwa njia ya amani. Kitu kinachotia matumaini ni kwamba siyo Ahmadinedjad aliyezungumzia kutumia utoaji wa mafuta kama silaha lakini aliyesema hivyo ni Khamenei. Huenda Iran inataka kupewa zaidi kwa kuacha kutengeza silaha za kinyuklia.” - Haya ni maoni ya “Leipziger Volkszeitung”.
Gazeti la “Die Welt” linajihusisha vile vile na hotuba iliyotolewa na kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ambayo ilitishia kuvuruga ugavi wa mafuta kutoka eneo la Ghuba. Gazeti hili limeandika:
“Kwa kusema hivyo, Khamenei anaweza kuwavutia wafuasi wake. Lakini anashindwa kuzichokoza nchi za Magharibi. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bibi Rice ana sababu mbili kwa kutokuwa na wasiwasi mkubwa. Kwanza: Ikiwa Iran itasimamisha utoaji wake wa mafuta itapoteza karibu mapato yake yote. Na pili: Kuvuruga ugavi wa mafuta kutoka eneo la Ghuba ndiyo sababu maalum kwa kuanza vita. Hivyo serikali ya Washington haingehitaji sababu nyingine kuishambulia Iran.”
Kwa maoni ya gazeti la “Kölnischer Stadtanzeiger”, tishio la Ayatollah Khamenei halina msingi. Limeandika:
“Wakati Iran inashurutishwa zaidi, inajaribu kujilinda dhidi ya jumuiya ya kimataifa. Lakini tishio lake haliaminiki. Kwani asilimia 80 ya bajeti yake Iran inategema mapato ya mafuta. Kwa kusimamisha ugavi wa mafuta, Iran ingejiathiri yenyewe!”
Mzozo wa Iran unalihusisha pia kombe la dunia la kandanda ambapo timu ya Iran itashiriki. Katika gazeti la “Badische Zeitung” tunasoma yafuatayo:
“Hatuwezi na hatufai kumzuia Ahmadinedjad kuitembelea Ujerumani. Lakini tunaweza kuandamana, kumuonyesha mabango na kumuambia kwa njia hiyo kwamba hatukubaliani na sera yake. Mchezo wa mpira haihusishwi na siasa – la hasha: Si kweli!”