Trump na timu yake wagawanyika kuhusu ujumbe kwa Iran
26 Machi 2025Utawala wa Trump umeweka masharti makali ya kutaka Iran ivunje kabisa mpango wake wa nyuklia huku ukiashiria uwezekano wa kulegeza msimamo.
Trump mwenyewe alikiri Machi 7 kwamba alimwandikia barua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, akimwalika kwenye mazungumzo, lakini pia akimwonya kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi endapo atakataa.
Hatua hii inafuatia kurudishwa tena kwa sera kali ya vikwazo, maarufu kama "maximum pressure," licha ya Trump kudai kufanya hivyo kwa shingo upande kutokana na ushawishi wa washauri wake wenye msimamo mkali.
Steve Witkoff, rafiki wa karibu wa Trump ambaye amekuwa mjumbe wake maalumu katika masuala ya kimataifa, hivi karibuni alidokeza uwezekano wa maelewano na Iran, akitaja pendekezo la Trump kuhusu mpango wa uthibitishaji wa kutengeneza silaha za nyuklia, unaofanana na mkataba uliofikiwa na Obama mwaka 2015.
Soma pia: Masoud Pezeshkian: Nini cha kutarajia kutoka kwa rais mpya wa Iran
Hata hivyo, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Mike Waltz, alikanusha haraka akisisitiza lengo lao bado ni "kuvunjwa kabisa kwa mpango huo."
Nafasi ya kidiplomasia na hatari ya kijeshi
Wachambuzi wanaona kuwa msimamo mkali wa Marekani hautafanikiwa kuitisha Iran katika meza ya mazungumzo. "Wairani hawatakubali kujadiliana huku wakiwa wamewekewa bunduki kichwani," alisema Ali Vaez kutoka Shirika la ufuatiliaji wa mizozo la International Crisis Group.
Hata hivyo, wachambuzi wengine kama Alex Vatanka wa Taasisi ya Mpango wa Mashariki ya Kati, wanaona Iran inaweza kutumia fursa hii kufikia makubaliano rahisi ambayo yanaweza kumpa Trump mafanikio ya kisiasa, kama vile ununuzi wa bidhaa za Marekani baada ya miaka mingi ya vikwazo.
Soma pia: Khamenei asema vitisho vya Trump kwa Iran "havitofika popote"
Jitihada za kidiplomasia za Trump zinakuja wakati Iran ikiwa katika nafasi dhaifu baada ya washirika wake Hamas na Hezbollah kushindwa vibaya katika mapigano ya karibuni na Israel.
Aidha, Syria chini ya Bashar al-Assad, mshirika mwingine mkuu wa Iran katika kanda, ilianguka Disemba mwaka jana. Hali hii inaongeza uwezekano wa Marekani na Israel kutumia nguvu za kijeshi kama njia ya kuishinikiza Iran zaidi.
Chanzo: AFP