Timu 8 kati ya 32 zimeaamua maskani zao kwa Kom,be la dunia,Ujerumani.
2 Desemba 2005Jumamosi hii huenda hatima ya mtaliana Giovanni Trapatoni,kocha wa stuttgart ikaamuliwa iwapo kwa mara nyengine –Stuttgart, itateleza katika changamoto yake na mabingwa Bayern Munich.
Stuttgart inacheza nyumbani katika Daimler-Stadium,lakini Munich, imeshinda mapambano yake 12 hadi sasa msimu huu kati ya yote 14.Trapattoni aliwahi kuwa kocha wa Bayern Munich alipowaongoza kutwaa ubingwa 1997. Stuttgart ina rekodi mbaya msimu huu, kwavile wameshinda mara moja tu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani na wako pointi 19 nyuma ya mabingwa Bayern Munich.Kwahivyo, Stuttgart na hatima ya Giovanni Trapattoni huenda ikaamuliwa baada ya firimbi ya mwisho jioni hii.
Munich imepanua mwanya wa pointi 6 kutoka Hamburg huku zikibakia mechi 3 kabla mapumziko ya wiki 6 kwa siku-kuu za X-masi na mwaka mpya.Hamburg inacheza leo na FC Cologne na Cologne, inahitaji pointi 3 kujiokoa kujiunga na safu ya timu 3 zinazoweza kurejeshwa daraja ya pili.Bremen wako pointi 8 nyuma ya munich na nahodha wao Frank Baumann anaungama kuziba mwanya huo si kazi rasisi.
Changamoto nyengine jioni hii :Borussia Dortmund ina miadi na Hannover,Kaiserslauten inacheza na Franlfurt,Bremnen na duisburg,Bielefeld ina miadi na Schalke.Kesho Bayer Leverkusen itaumana na Berlin wakati Mainz ina miadi na Wolfsburg.
Inayokamilisha kalenda ya leo lakini, ni Nuremberg na Borussia Monchengladbach.
Borussia lakini inavutana na stadi wake kutoka Brazil:Giovane Elber.Elber amepigwa faini ya kitita cha Euro 10.000, pia ameonywa achunge tabia yake na ulimi wake.Hii inafuatia Elber kumtuhumu kocha wa Borussia Mönchengladbach, Horst Koeppel kusema uwongo.Elber aliliambia gazeti moja kuwa kocha Hoeppel alimuambia hatacheza katika mechi ya jumapili iliopita dhidi ya Hertha Berlin kwa sababu za mbinu ya kimchezo.Baadae akawaambia maripoti kuwa Elber si fit kucheza na hivyo hakusema kweli.
Elber mwenye umri wa miaka 33,ambae aliibuka mtiaji mabao mengi katika Bundesliga alipokua akiichezea Bayern Munich, amechezeshwa mara 4 tu msimu huu na hakutia hata bao moja.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,stadi wa Manchester united Ruud van Nistelrooy aliwaonya wenzake kucheza uzuri zaidi na kutamba nyumbani ikiwa Manchester yataka kuziba mwanya wa pointi kati yake na mabingwa Chelsea.Manchester iko pointi 10 nyuma ya Chelsea na ingawa wameshinda mechi 6 nje ya Manchester,ushindi wao mwezi uliopita dhidi ya mabingwa Chelsea ulikuwa wapili tu nyumbani.
Tugeukie sasa Kombe lijalo la dunia nchini Ujerumani:
Nusu mwaka tu ikisalia kabla ya firimbi kulia kuanzisha Kombe lijalo la dunia na mwishoni mwa wiki ijayo kura itapigwa mjini Leipzig, kugawa timu hizo 32 katika makundi 8 mbali mbali,baadhi ya timu zimeshachagua wapi zitapiga kambi zao hapa Ujerumani kwa Kombe la dunia:
Hadi sasa lakini ni timu 8 tu zilizoamua-Ujerumani-wenyeji, Marekani,Argentina,Japan,Sweden,Holland na Iran.Hata muakilishi wa Afrika-Togo imeshaamua kuwa itapiga kambi katika mji mdogo wa Wangen huko Allgau,kusini mwa Ujerumani, wakati Iran itahamia Friedrichshafen.Mabingwa mara mbili wa dunia-Argentina watapiga kambi mjini Herzogenaurach,maskani ya viwanda vya zana za michezo Adidas na Puma.Argentina imependezwa na sehemu hiyo wakati ilipocheza huko katika Kombe la mashirikisho hapo Juni mwaka huu.Sweden itapiga kambi mjini Bremen.Japan itakuwapo hapa mjini Bonn.Holland itapiga maskani yake huko Hinterzarten karibu na Black Forest.
Marekani itapiga maskani katika mji wa Hamburg,mji wapili kwa ukubwa nchini Ujerumani.Wenyeji Ujerumani, watapiga maskani mji mkuu Berlin,ambako finali ya Kombe hilo la dunia itachezwa hapo julai 9.
Timu 24 zilizosalia kama vile mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil ,Uingereza,mabingwa 1966 na Ufaransa, mabingwa 1998 zimeamua kungoja hadi ijumaa ijayo desemba 9 itakapopigwa kura ya kugawa timu katika makundi 8 huko Leipzig.
Jaribio la mchezaji wa zamani wa taifa wa Ureno Edgar kuichezea Angola, nchi alikozaliwa katika Kombe lijalo la dunia,limekataliwa na FIFA-Shirikisho la dimba ulimwenguni.FIFA inadai stadi huyo hakutoa ombi lake kwa wakati unaotakiwa.Edgar anaeichezea klabu ya Malaga, nchini Spain,alitoa ombi lake hilo hapo Julai mwaka huu na hivyo alikosea kwa miezi 6 muda wa mwisho wa kuchukua hatua kama hiyo.Edgar aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Ureno miaka 7 iliopita katika mpambano wa kirafiki.
Kwavile, alizaliwa Luanda, Angola, Edgar,angeweza kubadili uraia na kuichezea Angola laiti angetoa ombi lake kwa wakati uliowekwa.Edgar aliwahi kuzichezea Benefica Lisbon na hata Real Madrid.Mechi yake ya mwisho wa ureno ilikua dhidi ya Msumbiji huko Ponta Delgado,hapo august,1998.
Kocha wa Ujerumani Jürgen Klinsmann, amebashiri wiki hii kwamba ni kwa bahati tu Ujerumani huenda ikatawazwa mabingwa wa dunia mwakani,lakini ni Brazil na Argentina ndizo mojawapo yaweza kutwaa kombe-alikisia Klinsmann.Ujerumani ilitoka sare 2:2 na Argentina katika Kombe la mashirikisho kati ya mwaka huu hapa Ujerumani kabla Argentina kuzabwa mabao 4-3 na Brazil katika finali .
Katika Kombe la Challenge Cup la Afrika mashariki na kati mjini Kigali,Ruanda, Zanzibar Heroes-timu ya Taifa ya Zanzibar imewasangaza mashabiki wake na maadui hadi sasa licha ya kwamba walipoondoka kuelekea Kigali, CAF-shirikisho la dimba la Afrika mjini Cairo, liliwanyima uanachama hadi kwanza FIFA imewapa uanachama.Hii lakini, haikuwazuwia kutamba mbele ya wenyeji Ruanda na baadae jirani zao Burundi.
Kinyan’ganyiro hiki kinavyoendelea hadi Desemba 10 itakapoamuliwa wapi Kombe hili mwaka huu litaelekea.Ethiopia ni mabingwa watetezi wanaotaka kurudi Adis Ababa na Kombe.Kenya Harambee Stars, iliwasili mashindanoni jumatatu badala ya kabla ya ufunguzi jumamosi.Kenya imekuwa na mabishano na wachezaji wake wanaodai fedha.Ni hali ilioonekana wakati wa kuania tiketi za Kombe la dunia na Kombe la Africa la Mataifa.CECAFA ikaamua kuiadhibu Kenya kwa faini ya dala 2000 amnbazo Kenya haikuweza kulipa na hivyo ikafunga virago kurudi Nairobi.