Thai na Cambodia zakubali kusitisha mapigano 'bila masharti'
28 Julai 2025Thailand na Cambodia zimekubaliana kusitisha mapigano baina yao bila ya masharti siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibra amesema.
"Cambodia na Thailand zilifikia maelewano ya pamoja kama ifuatavyo: Moja, usitishaji mapigano wa mara moja na usio na masharti masaa 24 kuanzia sasa, usiku wa manane wa tarehe 28 Julai 2025," Anwar alisema baada ya mazungumzo ya upatanishi nchini Malaysia.
Anwar, akitumia mamlaka yake kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), alisema kaimu Waziri Mkuu wa Thailand Phumtham Wechayachai na Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Manet wamefikia maelewano ya pamoja ya kuchukua hatua za kurejesha mataifa yao kwenye hali ya kawaida.
Viongozi wa Cambodia na Thailand walikutana siku ya Jumatatu huko Malaysia kwa mazungumzo ya kujaribu kufikia makubaliano baada ya siku tano za mapigano makali ya mpakani.
Raia wayakimbia makazi yao kutokana na mapigano
Takriban watu 35 wameuawa na karibu 200,000 wamekimbia makazi yao katika mapigano kati ya majirani hao wawili wa Kusini-mashariki mwa Asia, wanaozozania maeneo ya mpaka. Hatimaye mapigano yakazuka baada ya bomu kulipuka kwenye eneo la mpaka siku ya Alhamisi, huku pande zote mbili zikilaumiana.
Kujibu hilo, nchi zote mbili ziliwaita mabalozi wao na Thailand ilifunga vivuko vyote vya mpaka na Cambodia, na kuwaruhusu wafanyakazi wahamiaji tu wa Cambodia kurejea nyumbani.
Hata hivyo, kiongozi wa Thailand tayari alionyesha wasiwasi kuhusiana na utayari wa Cambodia kabla ya mazungumzo hayo ya Malaysia. "Hatuna uhakika na Cambodia, matendo yao hadi sasa yameonyesha kwamba hawana nia ya kutatua tatizo," Kaimu Waziri Mkuu wa Thailand, Phumntham Wechayachai aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kwenda Malaysia.
"Cambodia imekiuka sheria ya kimataifa, lakini kila mmoja anataka kuona amani. Hakuna anayetaka kuona machafuko yanayowaathiri raia."
Cambodia imekana vikali madai ya Thai ya kushambulia maeneo ya raia, na badala yake imesema Thailand imeyatia mashakani maisha ya raia wasio na hatia na kuitolea wito Jumuiya ya kimataifa kulaani uvamizi wa Thailand dhidi yao.