Tetesi za Kabila kuwasili Goma zazusha mivutano Kongo
22 Aprili 2025Kutokana na kuenea kwa taarifa bila kuwepo ushahidi kuhusu uwepo wa Joseph Kabila mjini Goma, na kwa kuzingatia kauli zake za hivi karibuni kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC, Caleb, mwanafunzi kijana wa Goma kama ilivyo kwa wakaazi wengi wengine, hakuweza kuficha hisia zake na jinsi alivyoshangazwa na taarifa hizo.
"Ni jambo la kuvunja moyo kuona kuwa rais wa zamani, ambaye sasa ni seneta wa maisha wa nchi aliyoiongoza kwa miaka 18, anaongoza kundi la waasi ambalo licha ya kaulimbiu ya ukombozi, linaua wananchi masikini; yote haya kwa lengo la kurudi madarakani. Ingekuwa vyema angengoja uchaguzi na kuona kama atachaguliwa na wananchi."
Taarifa za kuonekana kwa Joseph Kabila mjini Goma zimezua mijadala mingi. Lakini hakuna aliyemwona waziwazi rais huyo wa zamani. Hata hivyo, licha ya chama cha Kabila kukanusha taarifa hizo, raia bado hawajui ukweli ni upi.
Serikali ya Kinshasa yaghadhibishwa na tetesi za uwepo wa Kabila mjini Goma
Mjini Kinshasa, serikali iliyopoteza udhibiti wa mji huo wa mashariki haijatoa maelezo yoyote ya kina. Lakini haijaficha hasira yake, hali iliyosababisha wizara ya mambo ya ndani na ile ya sheria, kutangaza vikwazo dhidi ya Kabila wiki iliyopita, kutokana na taarifa ya kuwa Kabila yuko Goma chini ya ulinzi wa waasi wa M23.
Mawaziri wa wizara hizo mbili walitangaza kuanzishwa kwa mashtaka ya kisheria, kunyang'anywa mali za Joseph Kabila na kusimamishwa kwa chama chake cha kisiasa PPRD. Hatua ambazo Amani Kakimba, mfuasi wa PPRD, anasema hazina msingi, kwa sababu uwepo wa Kabila mjini Goma ni taarifa za uvumi.
"Serikali imetangaza maamuzi makubwa, lakini kwa bahati mbaya yametokana na uvumi kwa kuwa hakuna aliyeonyesha picha wala video kuthibitisha uwepo wa Kabila hapa Goma. Na hata kama angeamua kurudi Goma, ana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa Katiba inamruhusu." amesema mfuasi huyo.
Shughuli za baadhi ya viongozi wa chama cha Kabila zazuiwa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kongo pia imezuia mienendo ya baadhi ya viongozi wa PPRDwanaoshukiwa kushirikiana na Joseph Kabila katika kuhusika na uvamizi wa maeneo ya mashariki ya DRC na waasi wa M23.
Ferdinand Kambere, Naibu Katibu Mkuu wa PPRD, anapinga taratibu hizo.
"Tangu tulipoitwa kwa mara ya kwanza na ofisi ya kijeshi ya mwendesha mashtaka, ilikuwa tu taarifa tuliyoisoma. Lakini kuhusu kesi isiyo na msingi kama hii uvumi mtupu, inaanza kama taarifa, inakuwa uamuzi, na mwisho watu wanazuiwa kusafiri nje ya nchi. Tunapaswa kuarifiwa rasmi. Pia, kosa linapaswa kuwa la mtu binafsi, ni nini hasa kila mmoja anatuhumiwa nalo?" amehoji afisa huyo wa chama cha Kabila.
Madai ya kurejea kwa Joseph Kabila katika eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na jeshi la Rwanda, kunachukuliwa kama usaliti mkubwa na serikali ya Kongo.
Hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka kwa rais huyo wa zamani, ingawa wafuasi wake wamesema atalihutubia taifa hivi karibuni.