Tel Aviv. Waisrael wafanya maandamano kupinga kuwaondoa walowezi katika eneo la Gaza.
12 Agosti 2005Mamia kwa maelfu ya Waisrael wamefanya maandamano katikati ya mji mkuu wa Tel Aviv , wakipinga dhidi ya mpango wa kuwaondoa walowezi wa Kiyahudi kutoka katika eneo la ukanda wa Gaza.
Muda mfupi kabla ya maandamano hayo , jeshi la Israel lilifunga eneo la makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo linalokaliwa la Wapalestina kwa mtu yeyete ambaye si mkaazi wa hapo katika juhudi za kuzuwia watu wenye msimamo mkali kuweza kuzuwia mpango huo wa kujiondoa kutoka maeneo hayo.
Mpango huo unatarajiwa kuanza wiki ijayo.
Miezi kadha ya maandamano, vizuwizi vya barabarani pamoja na vitendo vya uharibifu vimeshindwa kutikisa nia ya waziri mkuu Ariel Sharon kuwaondoa walowezi hao kutoka katika makaazi 21 katika eneo la Gaza.
Katika mahojiano na televisheni ya Israel, rais wa Marekani George Bush amesema kuwa anaamini uamuzi huo wa kujiondoa kutoka Gaza utakuwa mzuri kwa Israel.