Teknolojia ya kisasa ya kilimo cha kumwagilia maji, Kenya
17 Aprili 2025Mto Thiba ni chanzo muhimu cha maji kwa wakaazi wa Mbeere Kusini. Ili kufanikisha kilimo cha kumwagilia, teknolojia ya kisasa ya kusambaza maji imewaletea tija.
Teknolojia ni rafiki kwa mazingira
Mashine hiyo ni rafiki kwa mazingira kwani haitoi moshi wala kelele. Mabomba yanasukuma maji kutoka Mto Thiba kwa kutumka nishati ya sola.
Wengi waliyoikumbatia teknolojia hiyo ni wanawake kwani ndio walinzi wa mashamba na mali ya jamii na walengwa wa mkakati wa kuinua jamii. Teknolojia haihitaji nguvu nyingi jambo linalowapa wanawake wepesi kuitumia.
Mashirika husika katika mradi
Ili kuileta huduma karibu na wakulima, shirika la Heifer linashirikiana na kampuni ya kijamii ya Sow Precise kuwafadhili kununua mashine hizo kwa bei nafuu. Sow Precise ni mmoja ya washindi wa shindano la 2024 la teknolojia la shirika la kimataifa la maendeleo ya miradi ya kilimo Heifer, Ayute.
Wakulima nao wanaweza kukodisha mashine kwa bei ndogo ya kumwagilia maji kwa kila eka ya shamba.
Heifer international lazindua mkakati wa kupanua miradi ya kilimo
Shirika la kufadhili miradi ya maendeleo la Ujerumani la BMZ ni moja ya washirika wa Heifer international. Ili kutimiza nadharia yao, shirika la Heifer limezindua mkakati wa miaka mitano kupanua miradi ya kilimo na maendeleo hususan ya wanawake na vijana katika kaunti 26.
Heifer international limefadhili miradi Kenya kwa miaka 44. TM, DW Mbeere kaunti ya Embu.