Teknolojia za usaidizi kwa watu wenye ulemavu bado ndoto
4 Juni 2025Asiya Mohamed, mwanariadha bingwa wa mashindano ya Olimpiki kwa walemavu kutoka nchini Kenya amepaza sauti kuhusu umuhimu wa teknolojia ya kisasa inayowasaidia watu wenye ulemavu.
"Si unajua sasa hivi tuko kwenye ule mfumo wa kiteknolojia, kama zile "services” zao zilikuwa tu zinasaidia mlemavu wa viungo, basi zifanywe zisaidie mlemavu ambaye haoni, na mlemavu ambaye hasikii", alisema Asiya.
Leo (04.06.2025) ikiwa ni siku ya maadhimisho ya teknolojia za usaidizi kwa watu wenye ulemavu, Kenya imeandaa warsha maalum inayowaleta pamoja wavumbuzi na kampuni kuu za kiteknolojia duniani, na pia wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali ya kutetea haki za watu wenye ulemavu, ili kuendeleza mchakato wa upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wote.
Isaac Mwaura ni msemaji wa Serikali ya Kenya, aliye na ulemavu wa ngozi. Anaeleza madhumuni ya kongamano hilo.
"Mwanzo, kule kujumuisha watu wenye ulemavu katika mkutano huu kutoka bara lote la Afrika, kwa sababu sasa hivi mawasiliano ya kisasa yamenoga sana upande ule. Na pia mambo ya Artificial Intelligence –AI- sasa hivi sio lazma kuwa na mkalimani ama mtu wa lugha ishara kama wewe una ulemavu wa kutosikia", alisema Mwaura kabla ya kuongeza :
"Jambo la pili ni kuhakikisha kwamba tuna sera kabambe ambazo zinajumuisha watu wenye ulemavu katika mawasiliano. Na jambo la tatu ni kuhakikisha ya kwamba tunawaondoa wale watu ambao wanawakejeli watu na kuwafanyia stihizai na kuwasimanga watu wenye ulemavu."
"Teknolojia ya kisasa ina umuhimu wa aina yake"
Warsha hiyo ya siku tatu imedhaminiwa na kampuni kubwa za kiteknolojia na mawasiliano zikiwemo Microsoft, Google na Wakfu wa mpango wa ufadhili wa Mastercard. Mashirika ya watu wenye ulemavu kutoka kote barani Afrika yanashiriki ili kujadiliana changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Chike Okogwu, mtetezi wa watu wenye ulemavu nchini Nigeria, amesema teknolojia mpya ni muhimu.
"Kwa watu wenye ulemavu, teknolojia ya kisasa ina umuhimu wa aina yake. Hebu nitazame, mimi natumia kiti cha magurudumu kinachotumia umeme. Inarahisisha mwendo na pia situmii nguvu kujisukuma. Kwa hivyo teknolojia mpya ni muhimu sana katika maisha ya watu wenye ulemavu."
Mojawapo ya changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ni ubaguzi pamoja na ukosefu wa kutekeleza haki za msingi zinazowatetea.
Asiya Mohamed kutoka Kenya ni mwanaspoti mwenye ulemavu na bingwa wa mashindano ya Olimpiki kwa walemavu.
"Huu mkutano unaleta hao wavumbuzi wa vitu tofauti tofauti vya kiteknolojia wazidi kuhakiki kuwa vitu ambavyo wanavivumbua view vinatusaidia zaidi sisi watu wenye ulemavu."
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu wapatao bilioni 2.5 kote duniani wanahitaji angalau matumizi ya teknolojia saidizi. Wadadisi wanasema teknolojia za usaidizi kwa watu wenye ulemavu bado ni ndoto kwa nchi maskini, ambapo kwa nchi za kipato cha chini wenye huduma hizo ni asilimia 3 pekee, ilhali kwa mataifa tajiri huduma hizo zinapatikana kwa asilimia 90 ya watu wenye ulemavu.