TEHRAN:Shirika la nishati ya Atomiki duniani kufanya mkutano mwingine juu ya Iran
10 Agosti 2005Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki la umoja wa mataifa limejitayarisha kuitisha tena mkutano wa dharura juu ya nia ya Iran ya mpango wake wa Nuklia.
Hapo jana shirika hilo lilifanya mkutano wake wa kwanza mjini Vienna lakini lilishindwa kukubaliana juu ya uamuzi wa Iran wa kuanzisha tena mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium.
Wakati huo huo rais Mahmoud Nejad wa Iran ameyakataa mapendekezo ya Umoja wa Ulaya.
Mjumbe wa Marekani katika shirika hilo la nishati ya Atomiki Gregory Schulte,ameutaja uamuzi wa Iran kuwa sababu inayozusha wasiwasi mkubwa na hivyo ametaka hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya Iran.
Serikali ya Iran inasisitiza kwamba inahitaji nguvu za Nuklia kwa matumizi yake ya kuzalisha nishati ya matumizi ya kawaida.Iran pia imesema ili kuweza kushirikiana na Umoja wa Mataifa itaviondosha vizuizi vilivyosalia vilivyowekwa na Umoja huo katika mtambo wake wa nuklia wa Isfahan baadae hii leo.