TEHRAN:Mzozo wa Iran juu ya mpango wa Nuklia waendelea kuchemka
21 Septemba 2005Msuluhishi mkuu wa Iran juu ya mzozo wa Nuklia amesema Iran huenda ikakataa kuwaruhusu wachunguzi wa shughuli zake za kinuklia iwapo itafikishwa mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Ali Larijani amesema Iran pia itafikiria kujiondoa kwenye mktaba wa kuzuia silaha za Kinuklia iwapo kile alichokiita kutumiwa kwa lugha ya kulazimisha kitaendelea.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki IAEA linaendelea kujadili juu ya sheria ya mpango wa Nuklia wa Iran.
Iran ilirejelea shughuli ya urutubishaji madini ya Uranium mnamo mwezi Agosti inashikilia kwamba mpango wake wa Nuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani na kwamba ina haki ya kujitengenezea Nishati ya Nuklia.
Nchi tatu za Umoja wa Ulaya Ujerumani,Ufaransa,na Uingereza pamoja na Marekani zinataka kuifikisha Iran mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwekewa vikwazo iwapo itashindwa kushirikiana na wakaguzi wa shirika la kudhibiti Nishati ya Atomiki IAEA: