Tehran. Rais wa zamani wa Iran aliyeshindwa katika uchaguzi adai kulikuwa na njama za kumchafulia jina lake.
26 Juni 2005Mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa pili wa rais nchini Iran amesema kuwa amekuwa mhanga wa kampeni chafu dhidi yake. Akbar Hashemi Rafsanjani amesema katika taarifa kuwa mamia ya mamilioni ya dola ikiwa ni mali ya raia wa nchi hiyo yametumika katika kuharibu jina lake pamoja na familia yake.
Hata hivyo , rais huyo wa zamani wa Iran amesema kuwa hatapeleka malalamiko mahakamani. Bwana Rafsanjani ameangushwa katika uchaguzi huo na mhafidhina meya wa zamani wa mji wa Tehran , Mahmoud Ahmedi – nejad ambaye amejipatia asilimia 62 ya kura. Kufuatia ushindi wake, Bwana Ahmedi-nejad mwenye umri wa miaka 49 amesema kuwa anapanga kujenga jamii imara ya yenye maendeleo ya Kiislamu nchini humo. Amesema pia kuwa atarejesha uadilifu wa kiroho katika jamii nchini humo.