TEHRAN. Rais aahidi mapendekezo mapya katika mpango wa kinuklia wa Iran
10 Agosti 2005Rais Mahmoud Ahmednejad wa Iran ameahidi mapendekezo mapya katika mpango wa kinuklia wa Iran ili kulainisha maelewano baina ya nchi yake na nchi za magharibi.
Shirika la nguvu za atomik la umoja wa mataifa tayari limeshafanya mkutano wa dharura mjini Vienna kujadili njia za kuilazimisha Iran isiendelee na mpango wake wa kinuklia.
Iran tayari imekiuka vitisho ilivyowekewa kwa kuanzisha tena mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium hatua ambayo inaweza kupelekea baraza la usalama la umoja wa mataifa kutowa amri ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kwa nchi hiyo.
Tehran inatetea hatua yake hiyo na kusisitiza kwamba mpango wake ni kwa ajili ya kuzalisha nishati ya kinuklia lakini nchi za magharibi zinahofia kuwa madini hayo ya Uranium huenda yakatumiwa kutengeneza silaha za atomik.