Tehran. Ndege ya abiria ya Marekani yatua Iran baada ya kupata matatizo ya kiufundi.
19 Juni 2005Ndege ya abiria ya Marekani ikiwa safarini kutoka Bombay India kwenda Amsterdam imetua kwa dharura mjini Tehran. Afisa wa safari za anga amesema kuwa abiria wote 255 pamoja na wafanyakazi wako salama na hakuna mtu aliyeathirika.
Marekani na Iran zimekuwa katika hali ya mvutano tangu mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran. Ndege hiyo ya shirika la ndege la Northwest ilitua katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran baada ya kutokea matatizo ya kifundi katika eneo la mizigo. Hakuna mahusiano ya safari za anga kati ya Iran na Marekani, licha ya kuwa ndege za kijeshi za Marekani zinaruka kupeleka misaada katika mji wa kusini wa Bam baada ya mji huo kuharibiwa na tetemeko la ardhi mwaka 2003.