Tehran. Mhafidhina mamboleo achaguliwa kuwa rais nchini Iran.
25 Juni 2005Bwana Mahmood Ahmedinejad mhafidhina mamboleo mwenye msimamo mkali , ambaye alikuwa meya wa jiji la Tehran ameshinda katika uchaguzi wa pili wa rais nchini Iran.
Amepata kura asilimia 61, kwa mujibu wa baraza la ulenzi la nchi hiyo. Rais wa zamani Akbar Hashemi Rafsanjani, ambaye ni mwenye msimamo wa wastani wa kidini, amepata kura asilimia 35.
Ahmedinejad, mwenye umri wa miaka 49, alifanya kampeni yake kwa kuzungumzia masuala ya watu masikini kwa kusema kuwa atajaribu kusambaza utajiri wa mafuta pamoja na kuirejesha Iran katika msimamo wa kidini. Matokeo hayo yanasitisha juhudi za mageuzi zilizoanzishwa katika mwaka 1997 na rais wa sasa anayemaliza muda wake Bwana Mohammad Khatami.
Viongozi wa upinzani wa Iran wanaoishi uhamishoni katika jimbo la Marekani la Califonia wamesema kuwa ushindi wa Ahmedinejad unaweza kuzusha hali ya kutokukubaliana na mgawanyiko ndani ya utawala wa nchi hiyo. Serikali ya Marekani imesema kuwa Iran iko nje ya msitari baada ya uchaguzi huo ambao imesema una dosari.