TEHRAN. Iran yateuwa mjumbe mwingine katika mazungumzo ya nuklia
8 Agosti 2005Shirika la habari la Iran limetangaza kuwa bwana Ali Larijani atachukua nafasi ya bwana Hassan Rohani kama mjumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya Nuklia na nchi za ulaya.
Bwana larijani ni muhafidhina aliye karibu zaidi na kiongozi wa kidini Ayatollah Ali Khamenei na anapendelea Iran iendelee na mpango wake kamili wa atomiki pamoja na mpango wa kurutubisha madini ya Uranium.
Wakati huo huo afisa mwenye cheo cha juu ametangaza kuwa kiwanda cha kurutubisha madini ya Uranium cha Isfahan kimeanza shughuli zake chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki.
Umoja wa ulaya umetishia kuipeleka Iran mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa ili kuwekewa vikwazo vya kiuchumi.
Iran inasisitiza kwamba mpango wake wa kinuklia ni kwa ajili ya kuzalisha nguvu za umeme lakini Marekani inashuku kwamba Iran inatengeneza silaha za kinuklia.