TEHRAN : Iran yataka mazungumzo ya nuklea yasiwe na masharti
11 Septemba 2005
Iran leo hii imesema haitosalimu amri kwa madai ya Umoja ya Ulaya kwamba isitishe tena shughuli zake kwenye mtambo wa kusindika uranium wa Isfahan na imesema kwamba mazungumzo yoyote yale na Umoja wa Ulaya juu ya masuala ya nuklea yanapaswa kuwa bila ya masharti.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manaouchehr Mottaki ameumbia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kuanza upya kwa shughuli hizo zilizositishwa za mtambo wa Isfahan sio sehemu ya agenda yao na suala hilo halipo kabisa kwao.
Iran ilianza tena shughuli zake hizo kwenye mtambo wa Isfahan mwezi uliopita hatua ambayo imekuja kusababisha kusambaratika kwa mazungumzo ya miaka miwili kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Tehran na kusababisha pia maafisa wa Umoja wa Ulaya kuionya Iran kwamba kesi yake hiyo huenda ikafikishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu.
Iran inaendelea kusisitiza kwamba mpango wake wa nuklea ni kwa ajili ya dhamira za amani na sio kutengeneza bomu la nuklea.