TEHRAN: Iran yaonya kutupilia mbali mapendekezo ya mataifa ya magharibi
30 Julai 2006Iran imeonya leo kwamba itatupilia mbali mapendekezo ya mataifa ya magharibi yanaoitaka ikomeshe mpango wake wa kinyuklia, ikiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litapitisha azimio la nyuklia dhidi ya Iran hapo kesho.
Azimio hilo lililowasilishwa na Ufaransa linaitaka Iran kusitisha urutubishaji wa madini yake ya uranium kufikia tarehe 31 mwezi ujao la sivyo iwekewe vikwazo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Iran, Hamid Reeza, amesema ikiwa azimio hilo litapitishwa, Iran itayaondoa mapendekezo yaliyowasilishwa na mataifa ya magharibi katika ajenda yake na kuanzisha sera mpya ya nyuklia.
Matamshi ya Reza ni jibu la kwanza rasmi kutolewa juu ya mapendekezo yaliyotolewa yanayoitaka Iran ikomeshe mpango wake wa kinyuklia.
Wakati huo huo rais wa Venezuela Hugo Chavez, anayeitembelea Tehran, ameitolea mwito Iran kuongeza uwekezaji katika raslimali yake ya mafuta na gesi. Chavez ameahidi kuisadia Iran bila masharti.
Akijibu rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad amemueleza Hugo Chavez kama kakake na mtu wa jamii ya wairan.