TEHRAN: Iran yabadili msimamo wake juu ya mpango wa nuklia
1 Agosti 2005Iran imebadili msimamo wake juu ya mpango wake wa kuanzisha tena shughuli zake za nuklia. Imesema itasubiri hadi kesho kabla kuendelea mbele na mpango huo.
Hapo awali serikali ya Tehran ilitangaza kwamba ingeanza shughuli hizo leo usiku ikiwa umoja wa Ulaya hautawasilisha mapendekezo mengine mapya hii leo. Shughuli za mwanzo zitaanza katika kiwanda kilichoko mjini Isfahan.
Iran imesema imelazimika kuchukua hatua hiyo kwa kuwa jumuiya ya Ulaya haijatoa ahadi zozote za kutia moyo katika mazungumzo kuhusu mpango huo wa nuklia.
Umoja wa Ulaya umesema leo kwamba itakuwa hatari kwa Iran kuanzisha tena shughuli zake za nuklia.
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, mataifa ambayo yamekuwa yakishiriki katika mazungumzo hayo, yamesema mapendekezo mapya yatatolewa baada ya wiki moja na ahadi zao zitakuwa za kuridhisha.