TEHRAN : Iran yaahirisha urutubishaji uranium
15 Mei 2005Iran imenuwiya kuanza tena shughuli zake za nuklia ilizositisha lakini inaahirisha kuchukuwa hatua hiyo kutowa nafasi ya duru mpya ya mazungumzo na Umoja wa Ulaya.
Hapo Ijumaa Iran iliachana na tishio lake la kuanza tena urutubishaji wa uranium hatua ambayo ingelikiuka makubaliano yake na mataifa matatu ya Umoja wa Ulaya.Uingereza,Ufaransa na Ujerumani ziliionya serikali ya Iran kwamba ukiukaji wa makubaliano yao ya kusistisha urutubishaji wa uranium utakuwa na taathira mbaya kwa nchi hiyo na kupendekeza kufanyika kwa mazungumzo mapya ya ngazi ya juu.
Wakati huo huo bunge la Iran leo limepiga kura kuipa wajibu serikali wa kutengeneza nishati ya nuklea hatua ambayo inapingwa na serikali ya Marekani kwa madai kwamba Iran inataka kutengeneza silaha za nuklea.
Muswada huo wa wabunge unasema Jamhuri ya Kiislam ya Iran inawajibika kuchukuwa hatua ya kuwa na teknolojia ya nuklia kwa ajili ya matumizi ya amani ikiwa ni pamoja na kifungu cha kutengeneza nishati ya nuklea kwa ajili ya uzalishaji wa megawati 20,000 za umeme.
Iran imekuwa ikisisitiza kwamba nishati yake ya nuklea ni kwa ajili ya mitambo yake ya kuzalisha umeme na sio kwa ajili ya kutengeneza silaha.